RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein leo ameungana pamoja
na vijana na wanafunzi walioshiriki katika Maadhimisho ya Sherehe za kutimiza
miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika chakula cha mchana alichowaandalia
kutokana na ushiriki wao katika sherehe hizo zilizofanyika Januari 12 mwaka
huu.
Hafla hiyo ilifanyika
katika viwanja vya Makao Makuu ya KVZ, Mtoni mjini Unguja, na kuhudhuriwa na
viongozi mbali mbali wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwemo makamo wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja na baadhi ya viongozi wa
vikosi vya SMZ.
Katika shukrani zake
Dk. Shein kwa vijana na wanafunzi hao zilizotolewa kwa niaba yake na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Issa Haji Ussi Gavu, alitoa pongezi kwa kushiriki
kikamilifu sambamba na kufanikisha vyema sherehe hizo zilizofanyika Januari 12,
2018 katika uwanja wa Amaan mjini Unguja.
Waziri Gavu alitoa
shukurani za dhati kwa walimu, wakufunzi, wasimamizi na washiriki wote
walioshiriki katika shuhuli za halaiki na kuzipamba sherehe hizo ambazo zilifana
kwa kiasi kikubwa kutokana na ushiriki wao.
Alieleza kuwa ushiriki
wao katika sherehe hizo ni dalili njema na mwenendo mzuri wa uzalendo kwa nchi
yao huku akieleza imani yake kuwa vijana hao wataendelea kuyaenzi na kuyalinda
Mapinduzi Matukufu ya Januari 12, 1964 kutokana na umuhimu wake mkubwa katika
maisha ya Wazanzibari na Watanzania wote kwa ujumla.
Alisisitiza haja ya
kuendelea kuilinda amani na utulivu mkubwa uliopo hapa nchini ikiwa ni
kielelezo madhubuti cha kuendelea kuyalinda na kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya
Januari 12, 1964.