Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu
wa Pili wa Rais Mohamed Aboud Mohamed alipokuwa akijibu maswali ya
wandishi wa habari katika Mkutano wake Ofisini kwake Vuga.
Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.
………………………………………………………………
Mwashungi Tahir na Fatma Makame/Maelezo Zanzibar
Waziri wa nchi Ofisi ya Makamo wa
Pili ya rais Mohammed Aboud Mohammed amesema uchumi wa Zanzibar unazidi
kuimarika kwa karibu ya asilimia saba na mfumuko wa bei bado upo kwenye
tarakimu moja na pato la Taifa linazidi kukua.
Ametoa maelezo hayo ofisini
kwake Vuga wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu
utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi Serikali ya awamu ya saba
kipindi cha pili cha uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza
la Mapinduzi Dkt Ali Mohammed Shein.
Amesema katika awamu hii kwa
ujumla harakati za uchumi zinaendelea vizuri na ishara zote za
kuimarisha uchumi katika mwaka huu wa fedha zinatoa sura nzuri za
mafanikio.
Akizungumzia suala la Muungano
amesema unaendelea kuimarika na vikao mbali mbali vya watendaji wakuu
wa pande mbili wakiwemo mawaziri vimeshafanyika na Makamo wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano ameshafanya vikao viwili vya kisekta kwa nia ya
kutatua changamoto zilizopo.
Waziri Aboud ameelezea kwamba
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekamilisha kazi ya kuipandisha hadhi
iliyokuwa Idara ya upigaji chapa na mpigaji chapa mkuu wa serikali na
kuwa wakala wa serikali wa uchapaji.
Aidha amesema kazi ya kufunga
mitambo mipya ya uchapaji imekamilika na mafundi wa kiwanda hicho
wanaendelea kupatiwa mafunzo ili kuimudu teknolojia mpya ya mitambo hiyo
ili kuongeza ufanisi na kuongeza upatikanaji wa huduma bora na kwa
wakati.
Sambamba na hayo Ofisi ya Makamo
wa Pili wa Rais kupitia Tume ya kitaifa ya kuratibu na udhibiti madawa
ya kulevya imepania kutoa athari za madawa ya kulevya kwa jamii.
Hivyo Tume hiyo imefanya kikao
maalum na maofisa na wapelelezi wa Jeshi la Polisi wa Mikoa na Wilaya
za Unguja kilichoongozwa na mkuu wa Mkoa Mjini Maghribi kuweka mikakati
dhidi ya uingizaji na usambazaji wa madawa ya kulevya .
Mh Aboud amesema ofisi yake
inashirikiana na Ofisi ya ukaguzi na mdhibiti mkuu wa Serikali kuendesha
zoezi la uhakiki wa wafanyakazi wa Ofisi ya Makamo ya Pili ya Rais na
Taasisi zake ili kubaini wafanyakazi hewa.
“Katika zoezi hili imebainika kwamba Ofisi yetu hakuna wafanyakazi hewa kama inavyobainika sehemu nyengine” alisema wazirihuyo.
Aidha amesema Ofisi ya Makamu wa
Pili wa Rais bado itaendelea kufanya kazi kwa bidii , ufanisi na tija
ili iweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
Amesisitiza kuwa mambo muhimu ya
kuzingatiwa hivi sa kwa nchi yetu ni kuimarisha uzalendo na kusimamia
matumizi bora ya ardhi kwani watukishirikiano katika masulala hayo
tutaweza kudumisha amani na upendo na kupiga hatua zaidi ya maendeleo