Alisema uhaba wa huduma za Umeme na Maji
Safi na Salama katika baadhi ya Mitaa Mjini na Vijijini umekuwa
ukiwasumbuwa sana Wananchi hasa akina Mama na kupelekea kutumia muda
wao mwingi kusaka huduma hizo badala ya nguvu zao kuzielekeza katika
miradi ya Maendeleo.
Balozi Seif Ali Iddi aliyasema hayo katika
muendelezo wa ziara zake alizoziandaa Maalum za kutembelea Majimbo mbali
mbali Nchini akiwa katika Jimbo la Mwanakwerekwe kujionea Mwenyewe
Maendeleo na Changamoto zinazowakabili Wananchi katika Majimbo hayo.
Balozi Seif akikagua Kituo cha Maji hapo
Mwanakwerekwe “C” ambacho Transfoma yake kwa sasa imezidiwa matumizi na
kuleta usumbufu wa upatikanaji wa Huduma za Maji sambamba na Umeme
katika eneo hilo alisema ushirikiano wa pamoja ndio jambo la msingi
linaloweza kuibua hitilafu zinazojitokeza na nguvu hizo hizo zikatumika
kuzipatia ufumbuzi changamoto hizo.
Alisema Mamlaka ya Maji Zanzibar na Shirika
la Umeme Zanzibar licha ya kupewa jukumu la kuhudumia Wananchi katika
Sekta za Maji na Umeme lakini pia Taasisi hizo zinaweza kufanikiwa
kukusanya mapato zaidi kama zitajenga mazingira bora zaidi ya
Miundombinu hasa katika Miji yenye ongezeko kubwa la Watu.
Mapema Meneja Uendeshaji wa Shirika la
Umeme Zanzibar Nd. Haji Silima alisema kutokana na usumbufu unaowakumba
Wananchi wa Maeneo ya kwerekwe na juhudi za Viongozi wao wa kulitafutia
ufumbuzi tatizo la umeme mdogo ZECO imeanza na hatua za awali za ujenzi
wa njia mpya za kupitishia Umeme kuelekea kwenye Transfoma ya
Mwanakwerekwe “C”.
Nd. Haji alisema mradi huo unaotarajiwa
kugharimu jumla ya Shilingi Milioni 70,000,000/-
zitakazotolewa na
Shirika lenyenye pamoja na Mchango wa Uongozi wa Halmashauri ya Wilaya
ya Magharibi “B” na Jimbo la Mwanakwerekwe utasaidia kuondosha tatizo la
Umeme katika eneo hilo pamoja na upande wa Mitaa ya Tomondo.
Meneja huyo Muendeshaji wa ZECO alimuahidi
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba kazi hiyo iliyochelewa
kumalizika kutokana na uhaba wa Vifaa pamoja na Fedha utakamilika Rasmi
Mnamo Tarehe 10 Febuari Mwaka huu.
Naye Mwakilishi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar
{ZAWA} Nd. Maulid Khamis alimuhakikishia Balozi Seif kwamba miundombinu
ya marekebisho ya mtandao wa Huduma za Maji safi na Salama katika eneo
hilo kwa iko vizuri.
Nd. Maulidi alisema Fedha za mradi huo
zimeshatengwa zinazofikia zaidi ya Shilingi Milioni 14,000,000/- na
kinachosubiriwa kwa sasa ni ufungwaji wa Transfoma Kubwa Mpya katika
Kisima hicho ili huduma za Maji safi irejee kama kawaida.
Balozi Seif katika ziara hiyo alikagua
eneo lililotengwa na Baraza la Manispaa la Wilaya ya Magharibi “B” kwa
ajili ya Maegesho ya Gari za Abiria zinazokwenda na kurudi njia ya
Wilaya ya Kusini Unguja hapo uwanja wa Jitimai ya zamani Magogoni.
Kituo hicho kimelenga kuondosha msongamano
katika eneo la Mwanakwerekwe pamoja na soko lake ambapo Gari za Abiria
zitalazimika kukaa zamu katika kituo hicho mpaka itapofika wakati wake
kwa ajili ya kutoa huduma za usarifi kwa abiria.
Balozi Seif alimalizia ziara yake kwa
kuangalia Jengo kubwa la Kisasa lililojengwa na Uongozi wa Jimbo la
Mwanakwerekwe kuwa Kituo cha Wajasiriamali cha Vijana wa Jimbo hilo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
aliupongeza Uongozi wa Jimbo la Mwanakwerekwe chini ya Mwakilishi wake
Mh. Abdulla Ali Kombo kwa juhudi iliyochukuwa ya ujenzi wa Kituo hicho
utakaopunguza wimbi la Vijana wasiokuwa na ajira ambao hupelekea kufanya
vitendo vilivyo nje ya maadili.
Akizungumza katika majumuisho ya ziara hiyo
baada ya kupokea changamoto mbali mbali zinazowakabili Wananchi wa
Jimbo la Mwanakwerekwe hapo Ukumbi wa Meli Nne Saccos Makamu wa Pili wa
Rais wa Zanzibar Balozi Seif alionya kwamba Kiongozi asiyekubali
kujikita katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka
2015/2020 atalazimika kuangaliwa kwa Tahadhari na Viongozi wa Kitaifa.
Balozi Seif alisema Chama cha Mapinduzi
kilitangaza Ilani na Sera zake kwa wananchi ilipokuwa ikiomba ridhaa ya
kuongoza Dolan a kufanikiwa kupewa jukumu hilo. Hivyo Viongozi wake
hawatokubali kuona baadhi ya watendaji wa Taasisi za Umma Serikalini
wanaichezea Ilani hiyo kwa kuwadhihaki Wananchi.
Kuhusu uvamizi wa maeneo yaliyotengwa na
Serikali kwa kazi maalum kana Kilimo na miradi ya huduma za Jamii Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliendelea kutahadharia Jamii kwamba
Serikali italazimika kuchukuwa maamuzi magumu wakati wa Utekelezaji wa
Ripoti ya Kamati iliyoundwa kufanya utafiti wa maeneo hatarishi.
Alisema Wilaya mbili za Magharibi “A” na
“B” zilizomo ndani ya Mkoa Mjini Magharibi ndizo zinazokuwa Muhanga
wakati wa Msimu wa Mvuza za Masika zinazosababisha mafuriko kutokana
na Ujenzi holela unaofanywa na baadhi ya Watu Wasiozingatia taratibu za
ujenzi.
Akigusia vitendo vya Ubakari vinavyooneka
kufuru ada Balozi Seif alitahadharisha wazi kwamba hakutakuwa na hatua
zozote zitakazochukuliwa na vyombo vya Kisheria iwapo Wananchi
watashindwa kufika Mahakami kutoa ushahidi pale wanapotakiwa kufanya
hivyo.
Alisema Kesi zinazotokana na vitendo vya
ubakaji na udhalilishaji wa kijinsia zinazoripotiwa kila kukicha hivi
sasa zimeshapindukia zaidi ya 200 hali inayolitia aibu Taifa katika uso
wa Dunia.
Mapema akitoa ufafanuzi wa changamoto
zilizowasilishwa na Wananchi wa Jimbo la
Mwanakwerekwe Mkuu wa Mkoa
Mjini Magharibi Mheshimiwa Ayoub Mohamed Mahmoud alisema Serikali
kupitia Mradi wa Huduma za Kijamii Mijini {ZUSP} inaangalia uwezekano wa
kuinyanyua zaidi Bara bara Kuu itokayo Mwanakwerekwe kuelekea
Makaburini.
Hatua hiyo ambayo kwa sasa iko katika hatua
za utafiti na uchambuzi imekuja kutokana na eneo hilo kukumbwa na
mafuriko wakati wa Mvua za Masika na hatimae kusababisha usumbufu wa
usafiri kwa Wananchi na hata wageni wanaotumia Bara bara hiyo kwa
shughuli za Kiutalii.
Alisema haipendezi kuona Barabara hiyo
inajaa Maji na kutuwama katika Bwawa la Mwanakwerekwe kutokana na
mafuriko ya Mvua na kuzuia shughuli zote za usafiri.
Akiitolea ufafanuzi changamoto ya Gari za
Ng’ombe na Punda zinazochafua mazingira katika Shehia ya Mwanakwerekwe
Mkuu huyo wa Mkoa Mjini Magharibi amewahakikisha Wananchi hao kwamba
zoezi la kuondosha mifugo hiyo litakamilika ndani ya Wikio Moja.
Mh. Ayoub aliwataka Wananchi kushirikiana
na Serikali ya Mkoa chini ya Kamati ya Ulinzi katika kuhakikisha kadhia
hiyo inayowatia hofu Wananchi inaondoka mara moja kutokana na wahusika
wa mifugo hiyo kutumia silaha za jadi wakati wa kujihami.