Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo (Kulia) pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar (ZFB) Omar Hussein Mussa wakibadilishana hati za makubaliano ya ushirikiano katika kuwajengea uwezo wanachama wa ZFB.
Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo (Kulia) pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar Omar Hussein Mussa wakizungumza na wajumbe wa Kamati ya Makubaliano kutoka Chuo cha Kodi (Kulia) na Zanzibar (kushoto) kabla ya kusaini hati za makubaliano katika chumba cha mikutano ITA.
Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo (wa pili kushoto), Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar (ZFB) Omar Hussein Mussa (wa pili Kulia) pamoja na Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala Tanzania (TAFFA) Stephen Ngatunga (wa kwanza kulia) katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya ushirikiano mara baada ya kusaini makubaliano ya kuwajengea uwezo mawakala wa Forodha Zanzibar.
(PICHA ZOTE NA OLIVER NJUNWA).
Na Oliver Njunwa, Dar es Salaam, 28 Januari, 2018
Chuo
cha Kodi (ITA) pamoja na Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar (ZFB),
vimeingia katika makubaliano ya kushirikiana katika kuwajengea uwezo Mawakala
wa Forodha Zanzibar.
Akizungumza
mara baada ya hafla fupi ya kutiliana saini makubaliano hayo, iliyofanyika hivi
karibuni katika Chuo cha Kodi jijini Dar es salaam, Mkuu wa Chuo hicho Prof.
Isaya Jairo amesema kwamba, makubaliano hayo ni muhimu kwani kila upande una watalaam
wa kutosha kuwasaidia Mawakala wa Forodha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
"ITA
inajivunia utaalam wake wa kufundisha na ZFB ina utaalamu katika masuala ya
kiforodha. Kwa hiyo wote kwa pamoja tutashirikiana ili malengo ya makubaliano
haya yaweze kufikiwa", alisema Prof. Jairo.
Prof.
Jairo aliongeza kuwa, katika makubaliano hayo, Chuo cha Kodi kitatoa mafunzo ya
muda mfupi na utaalamu wa masuala ya forodha kwa ZFB ili kuhakikisha kuwa
kunakuwa na Mawakala wa Forodha wanaofanya kazi kwa weledi.
Mkuu
wa Chuo cha Kodi pia amesema kwamba lengo la vyuo sio kupata fedha bali kutoa
wataalamu wa kutosha ambapo uwezo wa Chuo hupimwa kwa idadi ya wanafunzi wanaohitimu
na aina ya sifa walizonazo.
Aidha,
Prof. Jairo ameiomba ZFB kulinda hadhi ya jina la Chuo cha Kodi kwani kina jina
zuri kutokana na uzoefu wake wa kutekeleza makubaliano ya ushirikiano na
taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi.
"ITA
ina makubaliano na Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) pamoja na
Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) na kwa nchi za nje ina makubaliano na Malawi,
Zambia, Botswana na iliisadia Sudan Kusini kuanzisha Mamlaka ya Mapato nchini
humo", alisema Prof. Jairo.
Makubaliano
hayo yamefanyika katika Chuo cha Kodi Dar es salaam Ijumaa tarehe 26 Januari
2017 na kutiwa saini kati ya Mkuu wa Chuo cha Kodi Prof. Isaya Jairo na
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar Omar Hussein Mussa na
kushuhudiwa na Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) Stephen
Ngatunga.
Naye
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar ZFB, Omar Hussein Mussa
amesema kwamba makubaliano hayo ni msingi mzuri wa kupata Mawakala wa Forodha
wenye weledi na hivyo kupunguza changamoto zinazojitokeza katika tasnia ya
uwakala wa forodha.
"Makubaliano
haya ni jambo jema na yatakuwa endelevu kwa kuwa sisi tuko tayari kuhakikisha
yanaleta mabadiliko katika utendaji wa mawakala wetu wa Forodha", alisema
Bw. Mussa.
Kwa
upande wake Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania Stephen Ngatunga ambaye
alihudhuria hafla hiyo, amekipongeza Chuo cha Kodi pamoja na ZFB kwa
makubaliano hayo muhimu na kusema kwamba anafarijika kuona jitihada zake
zimefanikiwa kwani yeye alichangia kufanikisha suala hilo.
Katika
makubaliano hayo, Chuo cha Kodi kitasimamia kiwango cha taaluma itakayotolewa
kwa kuzingatia vigezo vya Baraza la Taifa la Mafunzo ya Ufundi (NACTE) na Tume
ya Vyuo Vikuu (TCU). Aidha, Chuo hicho pia kitasimamia udahili, mitihani, kutoa
walimu na vyeti baada ya kuhitimu wakati Chama cha Mawakala wa Forodha Zanzibar
kitapokea ada, kutoa wanafunzi, madarasa pamoja na vitendea kazi.
Chuo cha Kodi ni sehemu ya Mamlaka ya Mapato Tanzania ambacho kilipata ithbati kutoka Baraza la Taifa la Mafunzo ya Ufundi kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa watumishi wa TRA pamoja na wadau mbalimbali katika fani za Kodi na Forodha.