Na Saleh Ally
WEWE ni shabiki wa soka, na unaipenda
sana klabu yako na klabu yako ni mabingwa watetezi wa Tanzania Bara,
basi leo acha tuzungumze.
Kokote uendako duniani, hakutakuwa na
shabiki wa soka anayekubali kuishabikia timu ambayo haifanyi vizuri,
lakini kuna mashabiki wengi wapo katika klabu hazifanyi vizuri.
Huenda hili linaweza kuwa swali la
kwanza kujiuliza, kama kweli klabu, timu yake haifanyi vizuri, vipi huyu
shabiki anaendelea kubaki na kuishangilia?
Kunaweza kuwa na majibu mengi sana,
lakini jibu sahihi ni hivi; hakuna timu haijawahi kupoteza na hakuna
timu haijawahi kufanya vibaya. Kuna vipindi vya kupanda na kushuka
katika kila timu unayoijua duniani.
Kwamba kuna wakati ipo juu na wakati ipo
chini. Inapopanda kunakuwa na raha ya kupita kiasi kwa mashabiki wao
lakini kuna kipindi itashuka na ndicho kipindi cha kero kwa mashabiki
wake.
Wanaobaki ni wenye mapenzi ya dhati,
wale watu unaoweza kusema wana mioyo ya chuma kwa kuwa mapenzi yao kwa
timu husika ni yale ya dhati.
Kila mmoja anajijua ilikuwaje akaanza
kushangilia au kushabikia timu fulani. Huenda ni sababu ya baba au
wazazi wake, huenda sababu ya mchezaji fulani, rangi fulani na
kadhalika.
Kila shabiki amewahi kuonja uchungu wa kutokuwa na furaha au utamu wa furaha mambo yanapokuwa ni mazuri au magumu.
Kipindi hiki, lazima kitakuwa kigumu
kwako wewe shabiki wa Yanga ambaye huenda hujawahi kuambiwa kwa kuwa
kila anayekuambia anahisi atakuwa anakusaliti au utamchukia kwa kusema
kwake ukweli.
Kwa sasa Yanga iko katika nafasi ya tatu
katika msimamo wa Ligi Kuu. Tofauti yake na kinara Simba ni pointi
saba. Hili si geni, kumbuka msimu uliopita, Simba walifikisha hadi
tofauti ya pointi nane. Sasa, nani anaweza kuongoza Yanga yenye uimara
wa kufanya hivyo?
Sitaki kuingia katika kundi la waoga
wanaotaka kupendwa tu hata kama wanaona ukweli wao unaweza kuwa msaada,
hivyo wanachagua kuwa kimya. Kipindi hiki kinaweza kisiwe kizuri sana
kwa mashabiki wa Yanga kama ilivyozoeleka lakini pia lazima tukubali,
haiwezi Yanga ikawa na kero kila siku.
Mfano, wakati Azam FC inaonekana ni
tishio, inaweza kukwama kwa Yanga na furaha ikawa kwa Wanajangwani kesho
Jumamosi. Kama watapoteza na hali ilivyo, wakiyachukulia matokeo hayo
kama tatizo lisilobadilika, machungu yao yataendelea.
Yanga imebadili mfumo, kitu kibaya wengi
hawataki kukubali kwa kuwa wanazungumza au kufanya mambo kishabiki bila
ya kuangalia uhalisia wa mambo.
Chini ya Mwenyekiti Yusuf Manji, Yanga
ilikuwa na mfumo wa aina yake. Mfanyabiashara huyo alitengeneza mfumo
wenye heshima, usikivu na ubora wa mambo katika matumizi na usiku mkubwa
kutoka kwa kile alichoamini sahihi.
Heshima ya Manji, leo haiwezi kuwa ya
Clement Sanga kwa kuwa kama kuna fedha ilikosekana, mara moja Manji
alitoa kama msaada au mkopo na Yanga ikaendelea kufanya mambo yake
inavyotaka.
Hakuna fedha kwa ajili ya usafiri, Manji
anatoa, hakuna fedha sababu ya usajili, Manji anatoa. Kumbuka, wakati
hayo yakifanyika, furaha ya Mwanayanga ilizidi kusonga mbele na kuwa ya
leo, kesho, keshokutwa na zaidi.
Kwa sasa mambo ni tofauti, umeona fedha
za usajili zikiwemo za Donald Ngoma, Yanga ililazimika kwenda kukopa kwa
wadhamini na baadaye ikawa tatizo kubwa katika kusubiri ipate fedha
nyingine.
Hii ililazimisha kuchelewa kwa mishahara
na rundo la figisu. Kukiwa na taarifa hizi, lakini viongozi wa Yanga
nao kwa kuwa ni kazi yao kuitetea klabu yao, wakawa wanapambana kuziba
mashimo.
Katibu Mkuu Charles Boniface Mkwasa
anaweza kuwa mhanga wa mambo mengi, lakini mwisho watakuwa wanamuonea
kwa kuwa hiki ni kipindi kigumu kuongoza Yanga kuliko kingine.
Fedha za mishahara bado ziko juu na
wakati akiwepo Manji ingekuwa rahisi kusukuma mambo kwa kuwa kiongozi
mkuu anaweza kujifichia aibu yake ya kuepuka kuwa na deni la mshahara
miezi mitatu. Angalau kuchelewa mwezi mmoja.
Kwa sasa Mkwasa atatoa wapi fedha zote
hizo ili kuziba mapengo? Nakukumbusha kama Manji bado angekuwa Yanga,
leo huenda uamuzi wa kuachana na wachezaji wasio na faida kwa Yanga
ungepita. Leo haiwezekani kwa kuwa wakiachwa, stahiki zao zitalipwaje?
Kuhusiana na usajili mpya nani atatoa fedha?
Yanga haiwezi kumtegemea Manji milele.
Hiki ndiyo kipindi cha mpito kubadili mfumo kutoka ule wa Manji na
kuanzisha mwingine ambao utasonga mbele bila ya Manji.
Lazima mkubali, hii inahitaji muda na
inahitaji mabadiliko hata kama ni taratibu. Nani asiyejua kuwa kipindi
chochote cha mabadiliko huwa na maumivu yake?
Ndicho wanachopitia Yanga.
Viongozi wanaweza kupambana kupunguza
maumivu na ikiwezekana kufanya jambo kubwa zaidi, hili linawezekana.
Hili pia liko kwa wachezaji kama wakiamua.
La sivyo, maumivu yatakuwa ya milele na
hakutakuwa na nafuu kwa kipindi kirefu. Hivyo kwa shabiki wa Yanga,
lazima kujiandaa na kuweka akiba ya mambo ingawa, Yanga haiwezi kuwa
matesoni milele.