Chadema kimesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) inapaswa kulaumiwa kwa kuvuruga uchaguzi mdogo uliofanyika Agosti 12, 2018, kuorodhesha baadhi ya matukio iliyodai yalilenga kuwakandamiza wagombea wa chama hicho na wanachama.
Jana Alhamisi Agosti 16, 2018 chama hicho kilitoa taarifa kwa vyombo vya habari na kubainisha kuwa baadhi ya maeneo wagombea wake walienguliwa katika mazingira ya kutatanisha, hata walipojaribu kuhoji hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.
Chama hicho kimesema taarifa iliyotolewa na NEC kujibu tamko la Ubalozi wa Marekani kuhusu uchaguzi huo mdogo, haiakisi ukweli wa mambo na badala yake ilipotosha kuhusu kilichotokea kwenye mchakato wa uchaguzi huo.
Taarifa hiyo iliyotolewa na ofisa habari wa chama hicho, Tumaini Makene inasema NEC imeshindwa kusimamia uchaguzi uwe huru na haki, kutokana na ama kutokuwa na uwezo au kufumbia kwa makusudi hila na njama zilizokuwa zikifanyika kuharibu na kuvuruga uchaguzi huo.
“Jamii ya watanzania, jumuiya ya kimataifa na dunia nzima iliona na kushuhudia kupitia njia mbalimbali za upashanaji habari ikiwemo vyombo vya habari na mitandao ya kijamii jinsi ambavyo NEC ilishindwa kusimamia uchaguzi uwe huru na haki,” ilisema.
“Mathalani wagombea udiwani wa Chadema katika kata tano Tunduma walinyimwa fomu zao za kugombea kwa makusudi kabisa kisha fomu hizo wakapewa watu wengine (wanaodaiwa hawajulikani).”
Imesema, “kwa kutumia mbinu za kijinai zinazohusisha kughushi. Kama hiyo haitoshi wagombea wetu wakaanza kusakwa na kukamatwa na polisi na kubambikiwa tuhuma za jinai.”
Mbali na hoja hizo, Chadema imesema imeshangazwa na namna NEC ilivyohoji Marekani ilitumia utaratibu gani kupata taarifa ilizotoa kuwa uchaguzi uligubikwa na vitendo vya vurugu na ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi.
“Swali hilo la NEC linaibua swali jingine, je mamlaka zilizoharibu na kuvuruga uchaguzi huo zilifanya hivyo kwa sababu zilijua hakuna waangalizi wa kimataifa? Je zilifanya hivyo kwa sababu zilijua habari za matukio hayo hazitaufikia ulimwengu ambao hautakaa kimya,” imesema taarifa hiyo.
Agosti 15, 2018 NEC iliutaka ubalozi huo kuthibitisha inachokieleza juu ya uchaguzi huo, ikisema uchaguzi mdogo huwa hauna waangalizi wa kimataifa na kuhoji ubalozi huo umetoa wapi taarifa hizo na hayo iliyoyaona ni kwa kutumia utaratibu upi na sheria ipi.
Mpekuzi.