Imeandikwa na Haji Nassor, Pemba
ZIARA ya Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu kwenye chuo cha mafunzo Wete Pemba, imeanza kuzaa matunda, baada ya mtoto wa miaka miwili, aliekuwa na mama yake ambae ni mtuhumiwa wa dawa za kulevya, sasa amepata msamaria mwema na kutoka chuoni humo.
Mtoto huyo ambae amekaa rumande na mama yake zaidi ya miezi miwili, juzi Jaji Mkuu alimtembelea pamoja na wale wanafunzi wengine, na ndipo siku ya pili kuelezwa kuwa, tayari wanafamilia wa mtuhumiwa, kwenda kumchukua mtoto huyo.
Taarifa kutoka chuo cha Mafunzo Wete zinaelea kuwa, siku moja tu baada ya Jaji Mkuu kumtembelea mama huyo aliekuwa na mwanawe wa miaka miwili, sasa mtoto huyo ameshatoka na mama yake akiendelea kusubiri taratibu nyengine za kimahakama.
Aidha taarifa hizo zinaeleza kuwa, kwa vile mtuhumiwa huyo ni mgeni kisiwani Pemba, ilibidi wazazi wake watoke Unguja, na amekubali mwanawe alelewe na mzazi huyo, na sasa akibakia peke yake chumba cha mahabausu Wete.
Mwanamke huyo, juzi alimuelezea Jaji Mkuu kadhia iliomkuta hadi kuwekwa rumade na mwanawe wa miaka miwili kuwa, juu ya mumewake kukamatwa na dawa za kulevya kwenye nyumba wanayoishi, ndipo na yeye kukamtwa na kufikisha mahakamani.
“Nipo rumande tokea Febuari 13, na mwanangu kwa jambo ambalo sihusiki, huku akiangua kilio jambo ambalo lilimfanya na mtoto nae kulia,”alidai.
Siku moja tu baada ya ziara hiyo ya Jaji mkuu kwenye chuo cha mafunzo, siku ya pili mtoto huyo alifanikiwa kupata mlezi kutoka ndani ya familia yake kwa ajili ya kulelewa.
Awali Afisa Ustawi wa Jamii wilaya ya Wete Haroub Suleiman alisema, baada ya kupata taarifa ya kuwepo kwa mtoto huyo wa miaka miwili, walifika Chuoni hapo kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kumtoa mtoto huyo mahabusu.
“Ingawa kumbe taratibu zilitakiwa ziandaliwe na maofisa wa Idara ya usatawi wa jamii wa wilaya aliotoka mtuhumiwa, ambapo ni Chakechake, ndivyo alivyotueleza Mkuu wa Idara ya Ustawi wa Jamii Pemba, “alieleza.
Kwa upande wake Mkuu huyo wa Idara ya Usatwi wa Jamii kisiwani Pemba, Abdull Salum Mohamed, alisema ingawa awali mama huyo alionekana kuwa mzito kumtoa mtoto huyo, lakini taratibu za kumnyang’anya zingefuata hapoa baadae.
“Wengine hufanya kama kinga wanapokuwa na watoto chuo cha mafunzo au rumande na ukitafuta njia kwamba wawape wanafamilia huzua sababu, lakini mwisho sisi tusingekubali mtoto kubakia mahabusu au chuo cha mafunzo,”alieleza.
Tukio la kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo Mtumwa Ramadhan Himid, pamoja na mume wake Othman Abdalla Hamad, lilitokea Januari 25 mwaka huu, kwa kukutwa na kete 5115, baada ya kufanyiwa upekuzi katika nyumba anayoishi na kufikisha Mahakamani Febuari 13 ambapo kesi yake itaendelea tena Aprili, 30 mwaka huu.
Jaji Mkuu wa Zanzibar alianza ziara yake kisiwani Pemba April 17 na kumaliza April 20, ambapo pamoja na maeneo mengine pia alitembelea vyuo vya mafunzo Tungamaa, Wete, mahakama zote za mwanzo, wilaya na mkoa pamoja na Mahakama kuu.