Imeandikwa na Faki Mjaka-Maelezo
Jamii imetakiwa kuchukua tahadhari juu ya Ongezeko la Maradhi ya Matumbo ya kuharisha ambayo yameanza toka kuanza kwa msimu wa Mvua za masika katika Visiwa vya Unguja na Pemba.
Tahadhari hiyo imetolewa na kaimu Mkurugenzi Kinga Zanzibar Dkt Mohamed Dahoma alipokuwa akizungumza na Wanahabari kuhusiana na mwenendo wa Maradhi Zanzibar.
Amesema toka kuanza kwa msimu wa Mvua za masika Kituo cha ufuatiliaji wa mwenendo wa maradhi Zanzibar kimebaini zaidi ya Wagonjwa 700 wa Matumbo ya kuharisha.
“Mpaka sasa hivi hakuna Mgonjwa wa Kipindupindu Zanzibar iliyokuwepo ni kuongezeka kwa Maradhi ya Matumbo ya kuharisha..Ni wajibu wetu kuchukua tahadhari” Alisema Dkt Dahoma
Hata hivyo amesema hadi sasa hakuna Mgonjwa wowote aliyebaiwa kuugua Maradhi ya Kipindupindu Zanzibar.
Kutokana na hali hiyo Wizara ya Afya inatoa tahadhari ili Jamii iweze kujilinda ipasavyo dhidi ya maradhi hayo.
Amesisitiza kuwa Serikali kupitia Taasisi zake mbali mbali inaendelea na juhudi zake kuhakikisha taaluma ya afya kwa wananchi inawafikia na kutoa huduma stahiki kwa wale wote walioahirika na maradhi ya matumbo katika Vituo vya afya.
Dkt Dahoma ametoa Wito kwa jamii kuwapeleka katika Vituo vya matibabu wagonjwa wote watakaobainika kuharisha badala ya kuwatibia majumbani.
Amesema Serikali imejipanga kwa Vifaa Dawa na Madaktari wa kutosha kuhakikisha kila anayeathirika na maradhi hayo anatibiwa ipasavyo.
Akielezea kuhusua maradhi ya Matumbo ya kuharisha Dkt Dahoma amefafanua kuwa Maradhi hayo hutokana na mrundikano wa uchafu na husambazwa kupitia kinyesi kuingia katika chakula au maji.
Hivyo ni wajibu wa jamii kuhifadhi vyanzo vya maji na chakula dhidi ya maradhi hayo.
Aidha amesisitiza kunawa vyema kwa sabuni kabla na baada ya kula na kutumia maji yaliyochemshwa kwa ajili ya kunywa.
Zanzibar hukabiliwa na Mvua za Masika kila ifikapo mwezi machi na hadi May ambazo licha ya kuwa Neema kwa shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, huambata na mitihani ikiwemo maafa, maradhi ya kuharisha na kipindupindu.