Beki wa kushoto wa Yanga, Gadiel Michael, juzi
alikuwa shujaa wa timu hiyo kwa kufunga bao la umbali wa mita 25 katika
mchezo dhidi ya Azam, kisha akafunguka kuwa aliamini atafunga bao hilo
baada ya kumchungulia alivyokuwa amekaa golini, kipa wa Azam, Mghana,
Razak Abarola.
Katika
mchezo huo uliopigwa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Azam Complex, Yanga
ambao walikuwa wageni walifanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 huku
wakivunja rekodi ya timu hiyo kutokufungwa kwenye ligi ya msimu.
Beki huyo amefunguka kuwa awali
alipanga kutoa krosi kwa washambuliaji wa kati kabla ya kuamua kuupiga
moja kwa moja baada ya kumchungulia kipa alipokuwa amekaa.
“Nilijua
litakuwa bao kwa jinsi ule mpira nilivyokuwa nimeupiga kwa sababu awali
kabla ya kupiga baada ya ile pasi nilitaka kutoa krosi lakini
nilivyomuangalia kipa alipokuwa amekaa, nikaamua kuupiga moja kwa moja
na matokeo yake likawa bao zuri.
“Nashukuru kwa kuweza kufunga
haijalishi nacheza timu gani kwa sababu kama Azam nilikuwa nacheza
zamani siyo sasa na ilikuwa lazima niipiganie timu yangu kuhakikisha
inapata matokeo ya ushindi na ndiyo maana nilishangilia kwa kuwaambia
mashabiki wa timu yangu kelele zao hatujasikia na sikuwa na maana
nyingine,” alisema Michael.