Waziri wa Elimu na mafunzo ya amali Zanzibar Riziki Pembe Juma amesema Wizara haitomuonea haya kwa yeyote atakaegundulika kuhusika iwe kuchangia au kusababisha mitihani kuvuja sheria itachukuwa mkondo wake hata awe mtu wa karibu.
Mhe. Riziki Pembe ametoa kauli hiyo leo Disemba 4 katika ukumbi wa Mbadala Rahaleo wakati alipokuwa akizungumza na watendaji wa Baraza la mitihani kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuhusu kuvuja kwa mitihani na kukiri kuwa mitihani mengine itafanywa hapo tarehe itapotangazwa .
Aidha alisema tumeakhirisha kwa sababu tungeendelea nayo tungefanya maamuzi siyo ya haki kwa walokuwa hawakupata tusingeliwatendea haki.
Alisema iwapo atagundulika mtu yeyote hata awe na ukaribu wa aina gani Wizara haitoweza kumvumilia hatua za kisheria za utumishi zitachukuliwa ili iwe fundisho kwa wengine na tukio hili lisiweze kutokea tena.
Aliwaomba watendaji wote kuwa na ushirikiano ili ziondoke athari zilizojitokeza , pia suala la uzembe kama hili lisitokee tena watendaji wajiamini kwani walijikubalisha na walikula kiapo hivyo waache tamaa na wawe waadilifu hata Mwenyezi Mungu anahimiza uadilifu.
“Naomba mashirikiano katika utendaji mzima wa kazi ili uzembe huu usitokee tena kwani kila mtu alikula kiapo katika utendaji wake wa kazi muhali uondoke tutakwenda sambamba na nitakula nae sahani moja ”.Alisema Waziri huyo.
Nae Naibu Waziri Mmanga Mjengo Mjawiri alisema kiongozi yeyote aliyelelewa vizuri hakubali kwenda kinyume na kazi yake lazima atakuwa yuko makini na utendaji kazi zake.
Alisema hili ni tukio la aibu limetokea na hivyo tuwe makini suala hili lisijirejee tena kwani lineondosha uaminifu kwa jamii na hasara kwa Serikali , wanafunzi na walimu pamoja na wazee.
Na Mwashungi Tahir, Habari Maelezo Zanzibar.