Imeandikwa na HAJI NASSOR, PEMBA
KIJANA mmoja Samir Abdalla Ali miaka 19 mkaazi wa Machomane Chakechake, amekutwa akiwa ameshafariki dunia chooni, kwenye nyumba aliokuwa na mazoea ya kwenda, iliopo kijiji cha Tibegi Wawi na mwili wake kukutwa ukiwa unanin’ginia mithili ya aliejitundika.
Mamia ya wananchi wa Wawi na vijiji jirani, walikusanyika nje ya nyumba hiyo, baada kuwepo ripoti ya kijana huyo kukutwa chooni akiwa ameshafariki katika nyumba hiyo, na baadhi ya wapangaji waliomo ndani humo, wakiangusha kilio.
Mwandishi wa habari alishuhudia umati wa wananchi wakiwa wameizunguruka nyumba hiyo, ambapo ndugu na jamaa wa marehemu huyo, wakiwa nje kusubiri vyombo vyenye mamlaka vifike.
Baadhi ya wananchi wa eneo hilo waliokataa kutoa majina yao, walisema awali walimuona kijana huyo majira ya 1:40 asubuhi akipita mitaa ya Wawi, akitokea kijiji cha Machomane akaoishi na ndipo ghafla, wakasiki taarifa hiyo.
Walisema inawezekana sana kijana huyo hakulala kwenye nyumba alimokutwa ameshafariki, kwa vile mapema walimuona akitokea kwenye maakazi yake ya kudumu na kwenda Wawi alikokutwa na umauti huo.
Mjomba wa marehemu huyo, Alawi Kassim Said akitoa maelezo kwa vyombo vya ulinzi na usalama, alisema kijana huyo sio mgonjwa wa akili, wala mlevi bali alikuwa ni mtu na shughuli zake za kawaida.
Alisema hakuwa akijua sana ratiba zake, lakini amekuwa akilala eneo la Machomane na kazi zake wakati mwengine ni dereva wa gari mbali mbali, na kuhusu nyumba aliokuwa amekutwa ameshafarikia, alikuwa na mazoe tu ya kwenda.
“Mimi sijui na wala sina ripotia kwamba humo alimokutwa amaeshafariki ana mke au anal ala humo baadhi ya siku, taarifa hizo sina,”alifafanua Alawi.
Mapema daktari alieufanyia uchunguuzi mwili wa marehemu huyo Yahya Zaid Othman wa hospitali ya Chakachake, alisema hakumkuta na jeraha lolote wala mwili wake kutitigika mithili ya mtu aliepigwa marungu, bali ulikuwa katika mazingira ya kawaida.
Alisema kwa uchunguzi wake alibaini kuwa, marehemu alifarika muda wa saa moja iliopita tokea alipofika yeye majira ya saa 3:40 asubuhi na sio kweli kama alifarika zaidi ya saa tatu zilizopita.
“Marehemu inaonekana kama amefariki muda wa saa moja tu iliopita, maana hata viungo vyake, kama ulimi havijapiga weusi kuonesha amesfariki kwa muda mrefu,”alifafanua.
Kubwa ambalo marehemu lilimsababishia kifo chake ni jambo la kawaida ni kule kukosa “suffocation” yaani kukosa hewa ya oxygen kwa muda mrefu.
Alieleza kuwa eneo ambalo alimkuta ananin’ginia akiwa na kanga shingoni, baina ya miguu yake na ardhini ni wastani wamita tatu, jambo ambalo kama pengukuwa na mtu karibu na kumkata, asingepoteza maisha.
Mkuu wa wilaya ya Chakechake Rashid Hadid Rashid ambae alifika yeye na Katibu tawala wake, baada ya kusikia tukio, alisema, amepokea taarifa hiyo kwa mshituko mkubwa.
Alisema hilo ni pigo kuondokewa na kijana ambae ndio nguvu kazi kwenye taifa, ingawa yote hiyo ni mipango ya Muumba, na kuwataka ndugu, jamaa na marafiki wa marehumu kuwa na moyo wa subra.
“Kwakweli vifo vyote vinauma, lakini kama hivi vya kujitundika na hasa kuondokewa na kijana kama huyo wa miaka 19, huwa ni mtihani, lakini yote hayo ni mipango ya Muumba mwenyewe sisi na familia tumshukuru kwa hili,”alieleza.
Wakati huo huo Jeshi la Polisi baada ya kuukabidhi mwili wa marehemu kwa ndugu na jamaa wa marehemu kwa mazishi, wanaendelea kumuhoji mwanamke mmoja amabe anaishi kwenye nyumba hiyo, anaesemakana yuko karibu na marehemu.
Hili ni tukio la pili kwa mwaka huu kwa mkoa wa kusini Pemba, ambapo April 22 kijana Azani Abdall Suleiman miaka 28 wa Ole, alikutikana ndani ya msikiti wa Machomane Chakechake, akiwa ameshafariki huku, mwili wake ukining’inia .