Imeandikwa na Haji Nassor, Pemba
MFUKO wa maendeleo ya jamii Tanzania TASAF III, kisiwani Pemba, umefanikiwa kuwaungunisha kimawasiliano ya barabara wananchi wa zaidi ya 2000 wa kijiji cha Ziwani na Mipirani shehia ya Mlindo wilaya ya Micheweni mkoa wa kaskazini, baada ya kujenga barabara yenye daraja tatu ndogo.
Wananchi wa vijiji hivyo, walikuwa hawatembeleani kwa furaha hasa kipindi cha mvua, kwa vile kutoka kijiji kimoja kwenda chengine ilikuwa ni vigumu kupitika kutokana na mito ambayo ilikuwa na maji mengi.
Taarifa kutoka TASAF Pemba, zinaeleza kuwa, wanakaya waliomo kwenye mpango wa kuwanusuriwa na umaskini, ndio walioibua mradi huo, na TASAF kuukubalia na kuwapatia mtaalamu kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo.
Mratibu wa mfuko huo Mussa Said alisema, kukamilika kwa ujenzi huo uliohusisha pia daraja ndogo tatu, ni ishara kwamba wananchi hao kwa sasa watakuwa na uhakika wa safari zao hata siku za mvua.
Alieleza kuwa, wazo la wanakaya hao ni jema kwa wananchi wote wa shehia ya Mlindo na maeneo mengine, maana kabla ya kujengwa kwa barabara hiyo kwa kiwango cha kifusi, wakipata usumbufu wa kwenda katika shughuli zao.
“Hata wanafunzi ilikuwa siku za mvua kubwa, hawana uhakika wa kwenda masomoni, maana daraja tatu zilizomo kwenye kuunganisha barabara hiyo, zilikuwa zinazidiwa na maji,”alieleza.
Hata hivyo Mratib huyo wa TASAF Pemba, amwataka wananchi wa shehia ya Mlindo kuhakikisha wanaitunza barabara hiyo, ili iweze kudumu kwa muda mrefu, kwa ajili ya shughuli zao za maendeleo.
Msimamizi wa mradi huo kutoka shehia ya Mlindo Maryam Issa Omar, alisema karibu asilimia 90 ya ujenzi wa barabara hiyo imeshakamilika, na sasa wananchi wameshaanza kuitumia.
Alieleza kuwa, kutokana na TASAF kuikubali bajeti yao ya ujenzi wa daraja tatu ndogo “culvert” ndio hasa wananchi wanaotumia barabara hiyo, wamepata uhakika zaidi.
“Sisi ilikuwa safari zetu za kijiji kimoja kwenda chengine ni kipindi cha kiangazi tu, lakini siku za mvua kubwa inabidi upoteza muda wa kuzunguruka mbali, lakini sasa hatuna wasiwasi,”alieleza.
Baadhi ya wananchi wa wanaoishi shehia ya Mlindo walisema miradi kama hiyo, inayoihusu jamii yote, ndio hasa ambayo TASAF ilitakiwa kuipeleka kwa wananchi kwa wingi.
Omar Hamad Mati, alisema kwa sasa hata wao wenye gari za Ng’ombe wamenufaika nayo barabara hiyo, kutokana na shughuli zao za kiuchumi.
Mwanafunzi wa skuli ya Wingwi Hadia Juma alisema sasa watakuwa na uhakika wa kuhudhuria masomo kila siku, kutokana na kujengewa daraja hizo.
Shehia ya Mlindo wilaya ya Micheweni Mkoa wa kaskazini Pemba yenye walengwa wa kaya maskini 251 waliomo kwenye mradi wa TASAF, wamekuwa wakiendelea na kazi ya ujenzi wa barabara hiyo, na kujipatia ajira ya muda ambayo wanalipwa shilingi 2300 kwa siku.