Kikosi cha Yanga kimeendeleza rekodi mbovu msimu huu baada ya kupokea kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Mwadui FC katika mchezo wa ligi uliopigwa Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga.
Bao pekee la mchezo huo limewekwa kimiani na Awesu Ally mnamo dakika ya 19 ya kipindi cha kwanza kwa njia ya shuti kali la takribani mita 30 kutoka langoni kwa Yanga.
Matokeo hayo yanaweka rekodi mpya ya Yanga kushindwa kupata alama tatu katika michezo 9 ya mashindano yote msimu huu ikiwa ni pamoja na Kombe la Shirikisho Afrika, michuano ya Sports Azam Federation CUP pamoja na Ligi Kuu Bara.
Yanga inazidi kujiwekea mazingira magumu kumaliza ligi ikiwa nafasi ya pili kutokana na kupoteza mchezo wa leo dhidi ya Mwadui FC ingawa ina michezo miwili mkononi tofauti na Azam wanaowania nafasi hiyo.
Azam mpaka sasa wapo mbele kwa michezo miwili wakiwa wamecheza michezo 28 huku Yanga akicheza 26, na katika pointi Yanga amejikusanyia alama 48 na Azam akiwa ana 52.
Mchezo baina ya Yanga na Azam ambao bado hawajakutana kwenye mzunguko huu wa pili unaweza ukatoa taswira kamili ya nani atamaliza kwenye nafasi hiyo ya pili.