Mabalozi kupewa viwanja 54 bure Dodoma - NURU YA HABARI TZ

KWA HABARI ZA UHAKIKA ZA KITAIFA NA KIMATAIFA


HABARI MPYA

Home Top Ad

Responsive Ads Here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Wednesday, February 21, 2018

Mabalozi kupewa viwanja 54 bure Dodoma


BALOZI tano zilizopo nchini zimeanza safari ya kuhamia mjini Dodoma, ikiwa ni kuunga mkono hatua ya serikali ya kuhamia mjini humo. Balozi hizo ni za Brazil, China, India, Urusi na Namibia.

Tayari mabalozi wake wamekubali kufunga safari umbali wa kilometa 560 kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ili kuona viwanja walivyotengewa na serikali kwa ajili ya kujenga balozi zao.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Dodoma, Godwin Kunambi.

Amesema, manispaa imejiandaa kuwapokea mabalozi na watumishi wengine wa ofisi hizo kwa kuwapa maeneo ya kujenga.

Kunambi amesema, tayari viwanja 54 vimeandaliwa kwa ajili ya mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini, katika eneo kutakapojengwa mji mpya wa serikali mjini Dodoma.

Kunambi alisema viwanja hivyo vyenye ukubwa wa ekari 5.5 vitatolewa bure kama alivyoahidi Rais John Magufuli hivi karibuni, kwamba mabalozi watakaokuwa tayari kujenga ofisi zao mjini Dodoma watapewa viwanja hivyo bure.

"Viwanja hivyo ambavyo vitakuwa na hati zilizoandaliwa tayari, mabalozi watakuwa na nafasi ya kuchagua maeneo wanayotaka katika eneo hilo la Mji wa Serikali," alisema.

Kunambi akizungumza na mabalozi zaidi ya 61 Dar es Salaam hivi karibuni, aliwakaribisha kufika Dodoma na kuchagua viwanja hivyo ambavyo hatimiliki zimeandaliwa na zipo tayari kwa ajili yao. Pia aliwaonesha mpango wa mji wa serikali na mahali ambapo balozi zimepangiwa kuchagua viwanja hivyo kwa ajili ya kujenga ofisi, makazi kwa ajili ya watendaji wao.

Kunambi alisema, serikali ya mkoa na viongozi wa juu serikali, tayari imejiandaa kuwapokea mabalozi hao na hivi sasa inaandaa miundombinu ya maji na umeme ili kuhakikisha wanapotaka kuanza kujenga wanapata huduma hizo.

Tayari viongozi wa ngazi za juu serikali akiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wamehamia mjini Dodoma tangu Rais Magufuli alipotoa tamko la serikali kuhamia Dodoma, Julai, mwaka 2016.

Rais Magufuli aliwaalika mabalozi wa nchi mbalimbali kuungana na serikali ambayo imeamua kuhamishia Makao Makuu yake mjini Dodoma kwa kuwaahidi kuwapa viwanja bure kwa ajili ya kujenga ofisi zao.

Takwimu kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, zinaonesha kwamba kuna mabalozi 57 na nyumba za mabalozi 30 hivi hapa nchini.
HABARI KUU

Post Bottom Ad

Responsive Ads Here

HABARI