Kampuni ya Gushungu Holdings ya
rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe inatakiwa kuondoka kwenye
kipade kimoja cha ardhi kinachomilikiwa na shule moja la sivyo
ishtakiwe.
Kanisa la Reform linasema kuwa ardhi hiyo inamilikiwa na kundi la shule zake la Eaglesvale.
Wakili wa shule hiyo Rodney Makausi aliambia BBC kwamba mwaka 2016 serikali ilichukua ardhi hiyo kwa nguvu.
Serikali baadaye ikaondoa madai yake baada ya swala hilo kuwasilishwa mahakamani.
Lakini mwenyekiti wa bodi ya shule hiyo Enos Chomutiri anasema kuwa mahindi yalipandwa katika shamba hilo mwaka uliopita na bango kubwa la shule hiyo likaondolewa.
Mawakili wametaka kampuni hiyo kuondoka katika shamba hilo mwisho wa mwezi huu ama ishtakiwe.
Sio mara ya kwanza familia ya Mugabe imetuhumiwa kuchukua mali kwa nguvu.
Awali, familia hiyo imekuwa na mgogoro na wakulima masikini kuhusu ardhi moja inayodaiwa kuwa na utajiri wa dhahabu ,pia familia hiyo imetuhumiwa kwa kunyakua shamba moja linalozalisha ndimu zinazouzwa nje ya taifa katika eneo hilo hilo.