Kifusi cha udongo katika machimbo ya Mgodi usio rasmi, kimewafunika na kuwauwa wachimbaji wadogo watano katika wilaya ya Nyanh’hwale mkoani Geita.
Wachimbaji hao waliingia kunyume na utaratibu katika Mgodi uliopo chini ya leseni ya kampuni ya Accaccia, ambapo walipokuwa ndani ya Mgodi wanaendelea na uchimbaji , Novemba 29 mwaka huu saa mbili asubuhi kuta za mashimo matano zilianguka, kifusi cha udongo kikawafunika na kupelekea wachimbaji watano kupoteza maisha.
Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale, Hamimu Gweyama, amesema kuwa maiti tano zimeopolewa katika mashimo hayo na kukabidhiwa kwa ndugu zao kwajili ya taratibu za mazishi lakini watu wawili wamefanikiwa kuwaokoa wakiwa hai.
Ameongeza kuwa hadi sasa idadi ya watu waliokuwemo ndani ya mashimo hayo haijulikani kwasababu nivigumu kuwatambua kwani wachimbaji wadogo huingia katika mgodi huo bila kufuata utaratibu maalumu , licha ya Meneja wa mgodi huo Peter Ngalu, kusema kuwa, watu waliokuwemo kwenye Mgodi ni 10 ambapo watu 5 wameopolewa wakiwa washafariki dunia na wawili wakiwa hai.
Moja ya majeruhi Ntimba Gudi ambaye ameokolewa ameeleza kuwa shimo moja lilikuwa na watu watatu na shimo la pili lilikuwa na watu watano huku mashimo matatu yakiwa na mtu mmoja mmoja.
Na amefafanua chanzo kikubwa cha kuporomoka kwa mashimo hayo ni kwasababu shimo la jirani kulikuwa na uzembe wa kufunga magogo vizuri ya kushikilia kuta za mashimo na kupelekea kuta kuporomoka na baadae mashimo jirani yakaanguka kwani yanakaribiana sana kwa chini.