Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma akizungumza na Wakuu wa Wilaya pamoja na Wakuu wa Ulinzi na Usalama kuhusiana na maandalizi ya kuanza kwa mtihani wa darasa la nne,sita,kidatu cha pili pamoja na kidatu cha nne huko katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Vuga
Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Ayuob Mohamed Mahamuod akizungumza na wakuu wa Wilaya pamoja na Wakuu wa ulinzi na Usalama kuhusiana na maandalizi ya kuanza kwa mtihani wa darasa la nne,sita, Kidatu cha pili pamoja na kidatu cha nne (Picha na Kijakazi Abdalla Habari Maelezo)
Na Mwashungi Tahir. Maelezo Zanzibar. 31-10-2018. WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Amali Riziki Pembe Juma aliwataka walimu wanaosimamia mitihani wawe waangalifu katika usimamizi na kuepuka na mambo yasiyofaa kwenye vyumba vya mitihani na kwa wananfunzi wanaofanya mitihani.
Hayo amesema huko ofisini kwa Mkuu wa Mkoa Vuga wakati alipokuwa akizungumza na kamati ya ulinzi na usalama, wakuu wa Wilaya na Mikoa , Wakurugenziwa Wizara ya Elimu na waandishi wa habari kwenye kikao cha kuzungumzia kujiandaa na mitihani ya kidato cha nne darasa la sita na darasa la kumi na darasa la nne.
Alisema mitihani inaletwa na ina ulinzi mkubwa na usalama wa kutosha , na kuitaka kamati ya ulinzi na usalama iwe makini kuhakikisha mitihani yote inafanywa kwa usalama na kutarajia mitihani hiyo inafanyika kwa amani bila ya udanganyifu wowote .
Aidha akitoa tahadhari kwa walimu wanaosimamia mitihani waache udanganyifu na kuwataka wawe makini katika usimamizi wao wakibainika wamehusika na udanganyifu huo vyombo vya ulinzi na usalama itawachukulia hatua kwani tegemeo letu Zanzibar ifanye vizuri .
“Natoa tahadhari kwa walimu wanaosimamia mitihani mujiepushe na suala zima la udanganyifu mwalimu akibainika kajihusisha vyombo vya ulinzi vitafanya kazi yake na Wizara pia”.Alisema Waziri huyo.
Alisema tunatarajia wanafunzi wazuri wafaulu mitihani yao kwa akili zao ili waweze kuendelea hadi kidatu cha sita na kuingia kwenye chuo ili baadae tuje kupata wazalendo wazuri katika majukumu ya Serikali hapo baadae kwani wao ndio tegemeo la baadae .
Nae Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi ambae pia Kaimu wa Mkoa wa Kusini Ayoub Mohamed Mahmoud amewataka walimu wawasimamie wanafunzi katika mitihani yao vizuri na kujiepusha na udanganyifu kwani anatarajia matokeo mazuri katika Mkoa wake .
Akitoa wito kwa walimu aliwataka wasimruhusu mwanafunzi kufanya mitihani ikiwa hana sifa na akitokea mwalimu akimruhusu mwanafunzi kufanya mitihani basi sheria haitomuwachia zitamuondosha yeye.
“Iwapo mwalimu atamruhusu mwanafunzi kufanya mtihani akiwa hana sifa zinazostahiki kufanya mtihani basi mwalimu huyo ahakikishe atajiharibia sifa yeye”.Alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Pia alisema kila Mwalimu Mkuu na wasimamizi wa mitihani wawe waangalifu katika kutekeleza majukumu yao ya kazi na kuona wanafunzi wanafanya mitihani yao kwa usalama na utulivu.
Nae Mwenyekiti wa kamati ya mtihani Mkoa wa Mjini Hamida Mussa Khamis alisema kamati iliweza kusimamia utaratibu wa mitihani na imekwenda vizuri kama ilivyopangwa.
Alihakikisha ulinzi ulikwenda vizuri wala hakutokuwa na changamoto zozote na wala suala la udanganyifu hautotokea na tunaahidi mitihani itafanyika vizuri bila mivujo wala udanganyifu wowote na kuwataka wanafunzi wawe watulivu katika kufanya mitihani yao.
Imetolewa na Idara ya Habari Maelezo Zanzibar.