Na George Mganga
Aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa ameibuka na kusema kuwa sababu ya timu hiyo kupoteza dhidi ya Cape Verde ni kutumiwa kwa wachezaji wasio na uzoefu.
Mkwasa ameeleza kuwa Kocha Emmanuel Amunike aliingia na mbinu ya kuwachezesha wachezaji ambao hawana uzoefu na mechi za kimataifa jambo ambalo lilisababisha kutopata matokeo.
Mkwasa ambaye aliwahi kuingoza Stars miaka kadhaa nyuma, anaamini hilo lilikuwa anguka kubwa kwa Stars ambayo bado ina safari ya kusaka tiketi kuwania mashindano ya AFCON mwakani.
"Kitendo cha Amunike kuwatumia wachezaji ambao hawana uzoefu kimechangia kwa namna moja ama nyingine kushindwa kupata matokeo na hatimaye kupoteza kwa mabao hayo matatu" alisema.
Hata hivyo Mkwasa ameshauri ni vema Amunike akaangalia mapungufu yote yaliyojitokeza ili kuanza marekebisho haraka kuelekea mechi ijayo ya marudiano.
Mapungufu hayo Mkwasa anaamini yatamsaidia Amunike kukiandaa vema kikosi ili kukipa nguvu ya kupambana kuelekea kupta nafasi ya kucheza AFCON 2019.
Baada ya kupoteza mechi hiyo dhidi ya Cape Verde, timu hizo mbili zitarudiana tena jijini Dar es Salaam Oktoba 16 2018 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.