Na George Mganga
Uongozi wa klabu ya Simba kupitia Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano, Haji Manara, umefunguka kwa kuwajibu wale wanaopinga mabadiliko ya klabu hiyo kuingia katika mfumo wa kisasa kiuendeshwaji.
Akizungumza kupitia kipindi cha michezo 'Radio EFM', Manara amesema si busara kwa wanachama hao baadhi wanaopinga mabadiliko kuzungumzia pembeni wakati katika mkutano mkuu hawakuhudhuria.
Manara amesema kuwa mabadiliko hayo hayajaamuliwa na watu wachache bali ni wanachama waliohudhuria mikutano yote ya klabu kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa JK Nyerere waliridhia tangu ianze kufanyika.
Msemaji huyo ameeleza kushangazwa na watu wachache ambao wamekuwa wakiibuka mafichoni bila kujitokeza kwenye mkutano kupinga, badala ya kuhudhuria mikutano inayoitishwa ili kueleza hisia zao.
Kauli ya Manara imekuja kufuatia baadhi ya wanachama walioibuka na kupinga mabadiliko hayo wakidai kuwa katiba imefojiwa na hata mkutano wa dharura ulioitishwa juzi haukuwa halali bali batili.
Tayari Simba imekamilisha mchakato mzima baada ya kukutano katika mkutano uliofanyika Jumapili ya Mei 20 2018 na sasa katiba itapelekwa kwa Msajili wa serikali kusajiliwa na kitakachofuata ni kuandaa muundo tayari kwa mfumo kuanza.