WANACHOTAKIWA KUFANYA SIMBA KABLA YA KUIVAA NKANA FC - NURU YA HABARI TZ

KWA HABARI ZA UHAKIKA ZA KITAIFA NA KIMATAIFA


HABARI MPYA

Home Top Ad

Responsive Ads Here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Friday, December 07, 2018

WANACHOTAKIWA KUFANYA SIMBA KABLA YA KUIVAA NKANA FC

HABARI KUU




NA SALEH ALLY
KUIDHARAU Mbabane Swallows kwamba si timu nzuri ndiyo maana Simba wameifunga kiulaini sana na kujiaminisha kwamba Tanzania hatuwezi kuwa na timu zinazoweza kufanya vizuri katika michuano ya Afrika, itakuwa ni kujidanganya wenyewe.


Wakati mwingine mambo yanakwenda kihisia zaidi na wengi kuona kila kitu cha mpinzani ni cha hovyo, kibaya au hakifai.

Katika maisha ya kawaida hata kama una kila kitu, huwezi kujua kila kitu na kila kilicho kizuri hakiwezi kufanywa na wewe peke yako. Maana yake ni vizuri sana kuwafurahia, kuwakubali na ikiwezekana kuwapongeza wengine kulingana na wanachofanya.

Walichofanya Simba ni kitu kizuri kinachoashiria kwamba kipigo cha jumla ya mabao 8-1 walichoipa Mbabane Swallows ya Eswatini, ni mwanga kuwa wamepania kufanya vizuri na kweli walikuwa na hamu ya kufanya hivyo baada ya kuyumba na kukaa nje ya michuano hiyo kwa kitambo sasa.


Maana ushindi wa 4-1 nyumbani, halafu wakaboresha ushindi wa 4-0 ugenini. Kweli wana kikosi kizuri bila ya kujali wale Swallows walikuwa na majeraha, sijui walichelewa jambo fulani na kadhalika.

Hivyo kwa kuwa Simba ni ya Tanzania, inapaswa kupongezwa kwa kile walichokifanya kuanzia wachezaji, viongozi na hata mashabiki walioipa nguvu timu yao tokea mechi ya kwanza hadi ile ya pili.

Pamoja na hivyo, bado wanapaswa kukumbushwa sasa wanakutana na Nkana FC ambao wana tofauti kubwa na Mbabane Swallows lakini ni timu inayofungika na inawezekana kutolewa kama ilivyokuwa kwa Mbabane.

Simba inaondoka Eswatini na sasa inahamia Zambia. Hata kama kuna mabadiliko na maendeleo katika soka la Afrika lakini unapozungumzia mchezo wa soka, basi jirani zetu Zambia, wamepiga hatua zaidi na wanajulikana kwa ubora walionao.

Simba inajua ubabe wa Nkana FC dhidi ya Yanga na pia namna ambavyo ugumu wa mechi unakuwa zinapokutana timu hizo mbili katika mechi za kimataifa.

Nkana FC si timu ndogo kwa Zambia na hata Afrika kote. Kiwango chake kimekuwa cha saizi ya kati lakini ni timu yenye malengo na inajulikana kwa namna ambavyo imekuwa ikipambana na wakati mwingine ubabe wake dhidi ya timu za Tanzania.

Ukiangalia maandalizi ya mwanzo dhidi ya Mbabane, Simba hawakuwa na uhakika na nafasi yao ya kusonga mbele. Maandalizi yalikuwa mazuri na yenye umakini mkubwa.

Kwa maandalizi ya Nkana FC, Simba wanapaswa kufanya hivyo na ikiwezekana kwa kiwango cha juu zaidi kwa kuwa, ugumu umeongezeka.

Nazungumzia kuongezeka kwa ugumu kwa sababu tatu ambazo kimsingi Simba wapaswa kuzitazama na kutopuuza hata kidogo.

Mfano, sasa wanakwenda kucheza Zambia kama nilivyoeleza awali. Hakuwezi kuwa rahisi kwa kuwa wamepiga hatua na lazima wanajua kupambana na mechi za kimataifa.

Pili, kwa kuwa tayari Nkana wamefuzu mechi mbili za awali. Sasa wanakuwa wamefunguka zaidi na tamaa kubwa ya kufanya vizuri inakuwa imepanda. Hivyo wana hamu ya mafanikio zaidi kuliko ilivyokuwa kabla ya kucheza mechi ya kwanza.

Tatu ni tahadhari. Lazima watadumisha maandalizi yao, watajipanga zaidi kwa kuwa wanajua wanakutana na Simba iliyoshinda mabao nane. Hapa hakuwezi kuwa utani hata kidogo kutoka upande wao.

Simba nao pia wanaweza kuwa na mawazo hayo kama ya Nkana. Kikubwa waamini kama mipango ni thabiti, Nkana FC wanafungika na hakuna kisichowezekana hata kidogo.

Kingine ambacho Simba wanapaswa kukiona mapema ni suala la kujifunza. Pamoja na kushinda 8-1 kwa jumla, lazima kuna makosa wameyapitia. Hivyo kuna kila sababu ya kuyatumia kama mafunzo ili kuhakikisha Nkana wanakwenda nje ili kupitia wao katika Ligi ya Mabingwa Afrika, tuendelee kujifunza zaidi.

Post Bottom Ad

Responsive Ads Here

HABARI