Makala: Uvunjaji kokoto janga linalowatafuna watoto wa Mwambe Pemba - NURU YA HABARI TZ

KWA HABARI ZA UHAKIKA ZA KITAIFA NA KIMATAIFA


HABARI MPYA

Home Top Ad

Responsive Ads Here

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Monday, May 28, 2018

Makala: Uvunjaji kokoto janga linalowatafuna watoto wa Mwambe Pemba




Imeandikwa na Habina Zarazali, Pemba         
NI mwendo wa karibu saa 1:15 kwa gari kutoka Chake Chake hadi kijiji cha Mwambe, kilichoko Wilaya ya Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba.
Kijiografia kijiji cha Mwambe kina mandhari ya miamba ya mawe, lakini kina rutba tofauti na vijiji vingi vyenye hali kama hiyo.
Kijiji hiki chenye shehia tatu ambazo ni Jombwe, Mwambe na Mchakwe kina wakaazi 17,525 wakiwemo 8,150.
Kilimo ndio kazi kuu ya wanakijiji. Wanalima michungwa na migomba kwa ajili ya biashara na kunde na mbaazi kwa chakula. Mbali ya kilimo wenyeji pia wanajishughulikia na uvuvi, uchimbaji mawe na ukataji kokoto.
Kijiji hiki pia kimebahatika kuwa na skuli za msingi na sekondari, na kituo cha afya ambacho hutoa huduma kwa wenyeji.
Kwa sababu Mwambe ni kijiji cha mawe, watu wengi hasa wazee na watoto hujishughulisha na ukataji kokoto kwa ajili ya biashara.
Kazi ya ukataji kokoto imeajiri wengi wakiwemo watoto hali inayosababisha athari, ikiwemo kutokwenda skuli na matatizo ya kiafya, licha ya serikali na mashirika ya kimataifa kuchukua hatua mbali mbali kuidhibiti.
Zanzibar ambayo ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeridhia mikataba mbali mbali ya kuwalinda watoto, kama vile mkataba wa kimataifa wa haki za watoto (CRW) wa 1989.
Aidha mkataba wa Afrika wa haki na maslahi ya watoto (African Charter on the Rights and Welfare on the Child), iliopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) sasa Umoja wa Afrika (AU) mwaka 1990 ambao Zanzibar imeuridhia, umeeleza umuhimu wa watoto kulindwa dhidi ya ajira hatarishi.
Pia mkataba wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) namba 182 wa 1999 kuhusu mifumo mibaya ya ajira za watoto inasema ni kazi zozote zinazoweza kudhuru afya, usalama na maadili ya watoto, lazima zipigwe vita.
Na licha ya sera ya maendeleo ya vijana ya Zanzibar ya 2005 kueleza madhara ya ajira za watoto, bado hali ni tofauti katika kijiji cha Mwambe; watoto wanaendelea kujituma au kutumikishwa kwenye kazi ya ukataji mawe kwa ajili ya biashara.
Ajira hizi kwa watoto, zinapingana na sheria ya mtoto ya mwaka 2011, ambayo inakataka mtu au kampuni kumuajiri au kumtumia mtoto katika shughuli yoyote inayohatarisha afya yake, maendeleo ya elimu, akili, mwili na maadili.
Safari yangu ilinipelekea hadi Kwareni, ambako ndiko watoto wanakofanya kazi ya ukataji kokoto. Nilikutana na makundi ya watoto wadogo walio chini ya miaka 17 wakifanya kazi hii kwa ajili ya biashara. Kokoto hizi zinauzwa kwa wafanyabiashara na hutumika kwa shughuli za ujenzi wa nyumba za makazi na biashara.
Cha kushangaza watoto hawa ni wanafunzi wa madrasa moja ya Quran inayoitwa, Almadrasatul Rahman. Mwalimu wa madrasa hii, Ngwali Kassim Ali, anathibitisha kwamba watoto hao ni wanafunzi wa madrasa yake na wanafanya kazi hiyo ili wapate pesa za kuendeleza madrasa yao.
Anasema kazi hii wanaifanya kila siku ya Jumapili hadi wanapopata shehena moja ya gari ambayo huiuza kwa shilingi 100,000. Fedha wanazopata huzitumia kuendeleza madrasa yao.
Anakiri kwamba kazi hiyo huwaathiri watoto kiafya kutokana na vumbi na kujikata mikononi.
“Tunafanya Jumapili kwa sababu ndio siku ya mapumziko, haingiliani na siku za kwenda skuli,” anasema.
Hata hivyo, kwa mujibu wa mfumo wa elimu Zanzibar, wanafunzi wanatakiwa kwenda skuli kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, na huzitumia siku za Jumamosi na Jumapili kwa mapumziko na kucheza.
Mmoja ya watoto niliemkuta hapa, Fatma Haji (12), anasema kazi hii wanaifanya ili wapate pesa za kuendeleza madrasa yao.
“Wazazi ni wagumu kuchangia maendeleo ya madrasa, sasa ili kuhakikisha madrasa yetu inakua inatubidi tutafute pesa wenyewe na njia rahisi ni kukata kokoto kwa sababu wateja wapo,” anasema.
Lakini ukataji kokoto sio tu unaathiri maendeleo ya elimu ya watoto, pia una athari nyingi za kiafya kwa watoto ikiwemo matatizo ya kupumua na macho.
Lakini si wanafunzi wa madrasa hii tu waliopo hapa, wapo pia waliokufa hapa bila ya kuangalizi wazazi au walimu wao.
Khamis Makame (13), yeye amekuja na ndugu yake na kaka yake wa miaka 18. Hadi saa 7:20 nilipofika katika eneo hili, wameshajaza ndoo tatu za lita 20 na wanamalizia kukamilisha ya nne. Mkono wa Khamis umejaa kovu na suguru, mfano mtu anaefanya kazi za mateso.
Khamis anasema kazi hii wanaifanya kila siku wanaporudi skuli isipokuwa Ijumaa.
Mtoto Adam Kassim Ali (13) anasumbuliwa na tatizo la jicho hadi sasa baada ya kuingia kipande cha jiwe wakati akikata kokoto.
Anasema kazi anayofanya madhara, kwa sababu wakati mwengine anajikata vidole, anaingia mavumbi puani na machoni na baadhi yao wanapata matatizo ya macho kama alivyo yeye.
KWANINI WATOTO WANAFANYA KAZI HII?
Ali Makame (15) anaesoma kidato cha kwanza, mkaazi wa Kinundu, anasema anakata kokoto ili apate pesa za kusaidia familia yake.
“Maisha ya baba na mama ni magumu, baba amekuwa mzee na hana nguvu, hivyo hunilazimu kufanya kazi hii ili nipate pesa za kumsaidia. Kama sijakata kokoto unadhani nitapata wapi pesa za kumsaidia,” anahoji.
Juma Kombo (17) mkaazi wa Kibondeni, anasema siku nyengine hukatisha skuli akibakia porini kukata kokoto ili apate pesa ya kutumia skuli na kununulia nguo.
Kazi ya kukata kokoto haifanywi na watoto wa kiume pekee. Maryam Mtumwa Simai (14) anasema hubanja kokoto ndoo moja hadi mbili kwa siku na kuuza kwa shilingi 5,000 ambazo huzitumia skuli na nyengine kumpa mama yake.
KAULI ZA WANAKIJIJI                                   
Vuai Kheri Vuai (67) mkaazi wa kijiji cha Bwegeza, anasema ukataji kokoto una athari nyingi kwa watoto ikiwemo ugonjwa wa machao na kupumua lakini ni vigumu kuwazuia wanakijiji kutokana na umasikini.
“Hawa watoto hata waende skuli lakini akili zao zote ziko kwenye ‘mawe’ mara nyengine saa moja usiku unawakuta bado wanakata kokoto,” anasema.
Mboje Faki Juma (52), anasema huwakataza watoto wake wasifanye kazi hiyo, lakini wakati mwengine inakuwa vigumu kuwadhibiti.
Nassor Mbarouk Saidi (47) mkaazi wa Mbuyuni, anasema mbali ya mawe, kazi nyengine iliyoajiri watoto katika kijiji hicho ni uparaji na uuzaji samaki mitaani.
“Unakuta watoto wenye umri wa kwenda skuli wamejitwika sinia za dagaa wananadisha mitaani,” anasema.
SERIKALI INASEMAJE
Ofisa Ustawi na Uhifadhi wa Mtoto Wilaya ya Mkoani, Aisha Abdi Juma, anasema umaskini na kutengana kwa familia kumechangia watoto katika kijiji hiki na vyengine kutumbukia katika kazi zenye madhara.
“Baada ya wazazi kuachana familia inasambaratika, hali hii inawaingiza watoto kwenye maisha magumu na kuamua kufanya kazi za hatari,” anasema.
“Mtoto anapoona familia yake ni maskini huamua kufanya maamuzi mengine, kwa mikoa ya Tanzania Bara wanakuwa watoto wa mitaani lakini kwetu wanafanya kazi kama hizi, zote zina madhara,” anasema.
“Nimeshuhudia mtoto mwenye umri wa miaka saba mkaazi wa Shamiani Mwambe akikata kokoto huku mikono yake ikiwa na vidonda, nilipomuuliza aliniambia anataka pesa za kumsaidia bibi yake,” anasema.
Ofisa Mipango Kamisheni ya Kazi Zanzibar, Sara Ali Abdalla, anasema sheria ya mtoto ya mwaka 2011 haimzuii mtoto chini ya miaka 18 kufanya kazi, lakini zile zisizo na madhara na ambazo hazimnyimi haki ya kupata elimu.
Sheha wa shehia ya Jombwe Mwambe, Hakimu Khamis Omar, anakiri kwamba baadhi ya watoto ushiriki katika kazi ya ukataji kokoto na kukosa fursa ya kusoma.
Sheha wa shehia ya Mwambe, Hamadi Haji Faki, anakiri kwamba tatizo kubwa linalosababisha ongezeko la ajiria ya watoto katika kijiji hicho ni umaskini.
Kamishna wa Kazi kutoka Kamisheni ya Kazi Zanzibar, Fatma Iddi Ali, anasema kuna jitihada zinazochukuliwa na serikali na washirika wa maendeleo kukabili tatizo hilo, lakini bado watoto wanaendelea kufanya kazi za hatari.
Anasema serikali inatoa elimu na kusaidia kifedha familia zenye maisha magumu kupitia TASAF ili watoto wapate nafasi ya kurejea skuli.
Anasema juhudi hizo zimesaidia lakini bado katika baadhi ya vijiji kama Mwambe, kazi ya ukataji kokoto inaendelea.
WAHUDUMU YA AFYA
Mkuu wa kituo cha afya Mwambe, Shufaa Mohamed Ali, anasema, ukataji kokoto una madhara ya kiafya kwa watoto.
Anasema matatizo hayo ni pamoja na kuugua maradhi ya macho mara kwa mara, matatizo ya mapafu na kupumua.
“Watoto wengi wanaoletwa hapa wanakuwa na matatizo ya kifua na macho kwa sababu ya vumbi wakati wanapofanya kazi hii,” anasema.
MWALIMU MKUU
Mwalimu Mkuu skuli ya msingi Mwambe, Shaibu Othman Sagafu, anakiri kwamba watoto wengi wanafanya kazi ya ukataji kokoto ingawa kazi hiyo huifanya baada ya muda wa masomo.
SULUHISHO
Mkurugenzi Baraza la Mji Mkoani, Rashid Abdalla Rashid, anaeleza mikakati waliyojiwekea kuhakikisha tatizo hilo linapungua ikiwemo kushirikiana na wizara inayohusika na ustawi wa watoto ili kutoa elimu kwa wazee juu ya athari ya biashara hiyo.
“Hili ni tatizo na ni la muda mrefu hivyo ni vigumu kuliondoa kwa usiku mmoja, lakini tunajaribu kushirikiana na wizara na wazazi kutoa elimu juu ya athari za kazi hii,” anasema.
Ali Issa Shehe (32), anasema biashara hiyo ni sehemu ya utamaduni wao hivyo si rahisi kwa serikali kuidhibiti kama wananchi wenyewe hawajakubali kubadilika.
“Tukianzisha vikundi shirikishi na kupita katika maeneo ya machimbo kuwazuia watoto tunaweza kufanikiwa,” anasema.
Makame Mussa (40), anasema tatizo hilo linaweza kuondoka kama jamii itakubali kubadilika na kuacha kuwatumia watoto kwa maslahi yao

Post Bottom Ad

Responsive Ads Here

HABARI