Na Mwashungi Tahir . Maelezo Zanzibar.- 6-12-2018.
SERIKALI na Mapinduzi Zanzibar imejidhatiti kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto kwa nguvu zake zote, ambapo takwimu za mwaka 2017/2018 zinaonesha kuwa matukio 1, 091 yaloripotiwa kutoka jeshi la Polisi ukilinganisha na matukio 2, 449 yaliyoripotiwa mwaka 2016/2017.
Hayo ameyazungumza Makamo wa pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Balozi Seif Ali Iddi huko katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar wakati alipokuwa akiakhirisha mkutano wa kumi na mbili wa Baraza la Tisa la Wawakilishi .
Alisema takwimu hizi hazifurahishi hata kidogo hivyo ijapokuwa jitihada mbali mbali ya matukio haya yamepunguwa kwa mwaka 2017/2018 kwa hiyo inaonesha wazi tukijipanga vizuri tunaweza kabisa kupunguza vitendo hivi na pia hatimae kumalizika kabisa.
Pia alisema uzoefu unaonyesha kuwa vitendo vya ukatili na udhalilishaji hufanywa na watu wa karibu na familia na jambo la kusikitisha pale watu tunaowaamini kama walimu wa madrasa na Skuli kushiriki kwani matukio haya zaidi hufanywa kwa watoto kuliko watu wazima , ambapo takwimu kutoka Jeshi la Polisi zinaonyesha asilimia 88.8 ya matukio yaliyopokelewa yalikuwa ya watoto katika mwaka 2017/2018.
Balozi Seif alihimiza viongozi wa Baraza la Wawakilishi kuwa na tabia ya kupima afya zetu ili tupate kujitambua kwani bado ukimwi upo na unaathiri nguvu kazi ya Taifa na bado hauna dawa hivyo alitoa wito kwa wananchi kuchukua juhudi za makusudi kutumia ipasavyo huduma za upimaji na kutendea haki kauli mbiu ya mwaka huu “Pima virusi vya ukimwi ujue afya yako.
“Juhudi kubwa bado inahitajika kwa jamii katika kupunguza maambukizi tunatakiwa tuwe na tahadhari kubwa kwani maradhi haya hayana dawa.”Alisema Makamo wa Pili.
Pia alitoa onyo kwa wale wote waliohusika na kujihusisha kwenye kuvuja mitihani ya kidato cha pili kwa kusema ukitaka kuangamiza nchi basi uichezee elimu, udanganyifu wa mitihani ni miongoni mwa vitendo vya uhalifu wenye nia ya kuiangamiza nchi kimaendeleo.
Aidha alisema hakuna Serikali iliyo makini duniani itakayokubali kuchezewa elimu yake hivyo udanganyifu uliotokea wa kuvuja mitihani ya taifa uliotokea na kulazimisha Serikali kufuta mitihani hiyo haikubali lazima Serikali itachukuwa hatua kali dhidi ya wale wote waliohusika kwa uhalifu huo.
“Tutang’oa miti hata kama ni mikubwa kama mbuyu , miche mizizi na mbegu zinazosubiri kuchipua ili tukio hili lilotutia aibu katika Serikali yetu lisitokee tena” .Alisema Balozi huyo.
Aliwaomba wananchi wote wa Zanzibar washirikiane na Serikali katika kupiga vita uhalifu ambao ukiachiwa utaliangamiza Taifa , hivyo natoa agizo kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali kuchukua tahadhari ili udanganyifu wa mitihani kwa Zanzibar usitokee tena na kumpongea Waziri wa Elimu Mafunzo na Amali kwa kufuta mara moja mitihani hiyo baada ya kugundua imevuja.
Vile vile aliviomba vyombo vya ulinzi na usalama kufanya upelelezi wa kina na kuwapeleka Mahakamani wale wote waliohusika na udanganyifu wa mitihani hiyo.