Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,
akihutubia wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Jengo Jipya la Mahakama ya
Wilaya Mwanakwerekwe Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Mahkama
ya Wilaya Mwanakwerekwe kutatoa fursa kwa Mahakimu watakaoitumia Mahkama hiyo
kufanya kazi kwa bidii, weledi sambamba na kufuata maadili ya kazi zao.
Rais Dk. Shein ameyasema
hayo leo mara baada ya kulizindua jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mwanakwerekwe,
mjini Unguja baada ya kufanyiwa matengenezo makubwa.
Katika maelezo yake Dk.
Shein aliwaeleza Mahakimu kuwa hivi sasa watafanya kazi zao kwa furaha kwani
kila Hakimu atakuwa na ofisi yake tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma ambapo
walikuwa wakikaa zaidi ya mmoja na kuwa kikwazo katika utendaji wao wa kazi.
Alisema kuwa jengo hilo
litatoa changamoto kwao kwani hapatarajiwi kuwa na ucheleweshaji wa mashauri
ambao si utaratibu mzuri kwa mahakama.
Dk. Shein alisema kuwa
Mahkama ni chemchem ya kutoa haki na kila mtu anayekwenda Mahkamani anakwenda
kufuata haki, hivyo ni juu ya Mahakimu kufanya haki katika kesi wanazozihukumu
na wasikurupuke wala kubabaisha.
Alieleza kuwa mara
nyingi haki hukosekana kutokana na vitu vingi ikiwemo suala la rushwa ambalo
Serikali yake inalipiga vita kwa nguvu zote sambamba na kuwepo suala la kujuana
ambalo nalo husababisha mwenye haki kunyimwa haki na kupewa ndugu au rafiki.
Aidha, alieleza kuwa
Serikali ina wajibu wa kutayarisha sera na sheria zinazoimarisha na kukuza
fursa ya kupata haki nchini sambamba na kuwa na wajibu mkubwa wa kuziimarisha
na kuziwezesha Taasisi mbali mbali za Serikali zenye majukumu ya kutoa na
kupanua fursa za kupata haki.
Aliwasihi wananchi wote
wasichelewe kufika Mahkamani kudai haki zao pale wanapohisi wamedhulumiwa haki
zao na waepuke kwenda sehemu nyengine ambazo haziwezi kusaidia au kuweka
pembeneni uamuzi uliotolewa na chombo hicho.
Pia, aliwataka wananchi
washirikiane na wahusika mbali mbali hasa wanapotakiwa kutoa ushahidi katika
kesi za jinai zinazofunguliwa Mahkamani kuhusu kesi za ubakaji, udhalilishaji
dawa za kulevya na nyenginezo. “ushahidi ni jambo muhimu sana unaosaidia hukumu
ifanyike kwa haraka”,alisisitiza Dk. Shein.
Dk. Shein pia, alitumia
fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kushikamana na kushirikiana na Serikali
katika mapambano dhidi ya rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma, dawa za kulevya
na maovu mengine yanayodhorotesha maendeleo katika jamii.
Sambamba na hayo, Dk.
Shein alisisitiza juu ya jukumu la mahakama la kuwaelimisha wananchi juu ya
shughuli inazozifanya pamoja na mafanikio yanayoendelea kupatikana huku
akiuhakikishia umuhimu huo kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao katika
kuhakikisha zinajengwa mahakama za kisasa pamoja na kuwa na utaratibu wa kudumu
wa kuzifanyia ukarabati mahkama hizo.
Pamoja na hayo, Dk.
Shein aliiagiza Wizara ya Nchi Afisi ya Rais, Katiba, Sheria na Utumishi wa
Umma na Utawala Bora pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango kuhakikisha inajenga
haraka jengo la Mahkama Kuu huko Tunguu ambapo mnamo mwaka 2020 yeye mwenyewe
akalizindue tena si zaidi ya hapo kwani mda haupo.
Nae Jaji Mkuu wa
Zanzibar Omar Othman Makungu alisema kuwa uzinduzi wa Mahkama hiyo ni miongoni
mwa muendelezo wa sherehe za kuadhimisha Siku ya Sheria, Zanzibar kwa mwaka huu
wa 2018.
Alieleza kuwa uzinduzi
huo ni muhimu sana kwa sababu inabeba wananhi wengi wanaokuja kupata huduma
kutoka Wilaya ya Mjini na Magharibi ambapo kutokana na wingi wa kesi zilizopo
wamelazimika kuweka Mahakimu wengi ili waweze kuhudumia vyema wananchi.
Alisema kuwa kwa sasa
Mahkama hiyo ina Mahakimu wa Wilaya sita wanaume wanne na wanawake wawili na
Mahakimu wa Mahkama ya Mwanzo saba wanaume watano na wanawake wawili na kueleza
kuwa kutokana na wingi wa Mahakimu na uchache wa vyumba baadhi ya Mahakimu
walilazimika kutumia ofisi moja kwa Mahakimu wawili.
Hivyo, kutokana na hali
hiyo ndio walipokuja na wazo hilo la kuifanya upanuzi wa jengo kwa kuongeza vyumba,
ghala, vyoo na ofisi nyenginezo huku akieleza kuwa kukamilika kwa jengo hilo ni
furaha kwao lakini changamoto kwa Mahakimu wa Mahkama hiyo kwani sasa
watatakiwa kuonyesha jitihada zao za kazi za kusikiliza mashauri na kuyatolea
maamuzi kwa haraka.
“Uongozi wa Mahkama
utafuatilia kwa karibu sana shughuli za Mahkama hii ili kuhakikisha kuwa ni za
ufanisi. Mahkama hii itatoa nafasi nzuri ya kuwapima Mahakimu wetu katika
kuamua mashauri kwa usahihi na kwa wakati”,alisema Jaji Makungu.
Aidha, Jaji Makungu
alisema kuwa tatizo la udhalilishaji wa watoto na wanawake nalo ni miongoni mwa
kesi nyingi zilizofunguliwa katika mahkama kwa mwaka uliomalizika ambapo
takwimu zinaonesha kuwa katika mwaka 2017 zilipokelewa kesi 105 za
udhalilishaji Mahakamani Unguja na Pemba na kati ya kesi hizo 57 zilimalizwa na
zilitolewa hukumu.
Mapema Kaimu Mrajis wa Mahkama Kuu, Isaya Kayange akitoa taarifa
ya matengenezo ya jengo hilo alisema kuwa matatizo makubwa ambayo yalikuwepo
kabla ya matengenezo hayo ya hivi sasa ilikuwa ni uchache wa ofisi za kufanyia
kazi kwa kutumiwa na Mahakimu na wafanyakazi wengine, kuvuja kwa jengo na mfumo
mbovu wa majitaka na umeme.
Alisema kuwa kutokana na
ubovu wa jengo hilo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika mwaka wa fedha
2016/2017 ilitenga bajeti kwa lengo la kulifanyia matengenezo makubwa jengo
hilo na mnamo tarehe 20 Februari, 2017 wafanyakazi wa Mahkama hiyo walihama kwa
ajili ya kupisha ujenzi huo.
Kwa maelezo ya Kaimu
huyo Mrajis, alieleza kuwa ujenzi huo ulisimamiwa na Wizara ya Nchi Afisi ya
Rais, Katiba, Sheria na Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo mjenzi
aliechaguliwa kufanya kazi hiyo ni Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM),
ambapo gharama ya ujenzi huo ni TZS Milioni 176.4
Katika hafla hiyo
viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Seif Ali Idd pamoja na viongozi wengine ambapo kikundi cha Black Root
kinachoongozwa na msanii Makombora kilitumbuiza kwa mchezo wa kuigiza
unaoendana na masuala ya sheria pamoja na uzinduzi wa jengo hilo.