Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu ametoa siku 30 kwa mkandarasi wa SUMA JKT, aliyepewa kazi ya kujenga jengo la ofisi ya wizara hiyo katika mji wa serikali eneo la Ihumwa, Jijini Dodoma.
Amemtaka Mkandarasi huyo kufanya kazi usiku na mchana ili aweze kukamilisha ujenzi wa jengo hilo ndani ya siku hizo 30.
Ameyasema hayo mara baada ya kutembelea eneo hilo la ujenzi wa jengo la ofisi za Wizara hiyo linalotarajiwa kugharimu shilingi bilioni moja za kitanzania katika eneo la Ihumwa jijini Dodoma.
Aidha, Kanyasu amemtaka mkandarasi huyo wa SUMA JKT kuhakikisha anajenga jengo hilo kwa umakini, umahiri na viwango vya ubora wa hali ya juu vinavyokwenda sambamba na hadhi ya wizara yenye mchango mkubwa kwenye pato la Taifa.
Ameielekeza SUMA JKT wakati ikiendelea na maandalizi ya ujenzi wa jengo iwe inatoa taarifa kila siku kwa kila hatua inayofikia katika Ujenzi wa jengo hilo kwa Uongozi wa Wizara.
Awali, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Lusius Mwenda amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa eneo hilo litakalojengwa Ofisi za Wizara hiyo lina ukubwa wa Hekta 2. 27