Hayo yamebainishwa na Katibu mtendaji wa NECTA, Dkt. Charles Msonde ambapo amesema kuwa, watakaohusika na kukiuka kwa kanuni za mitihani watawajibishwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.
“Watahiniwa watambue kuwa kukiuka kanuni za upimaji au kufanya udanganyifu kutafanya wafutiwe matokeo yao yote, lakini pia Baraza halitosita kukifuta kituo chochote cha mtihani endapo litajiridhisha kuwa uwepo wake unahatarisha usalama wa upimaji wa taifa“, amesema Dkt. Msonde.
Wanafunzi wa kidato cha pili wameanza mitihani yao leo Novemba 12, kote nchini na watamaliza Novemba 23, huku wanafunzi wa darasa la nne wao wataanza tarehe 22 na 23 mwezi huu.
Hayo yanajiri ikiwa ni miezi michache tu tangu Baraza hilo lilipofuta matokeo ya darasa la saba kwa baadhi ya shule nchini kutokana na udanganyifu, ambapo shule zilizofutiwa ni, shule za msingi zote zilizopo ndani ya Halmashauri ya Chemba, pamoja na baadhi ya shule katika halmashauri ya Kondoa, Kinondoni, Mwanza jiji na Ubungo kwa kosa la kuhusika kwa kuvujisha kwa mitihani ya darasa la saba ikiwa ni kinyume na taratibu na kanuni za mitihani nchini.