Mjumbe wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali ameibuka na kumpinga Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, George Mkuchika, ndani ya klabu hiyo kutokana na sakata zima la uchaguzi ambao unapaswa kufanyika mwezi Januari mwakani.
Akilimali ameeleza kushangazwa na maamuzi ya Mkuchika na Baraza lake kuingilia majukumu ya Kamati ya Utendaji ambayo ilikubaliana vizuri na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufanyika kwa uchaguzi.
Mzee huyo amesema Baraza hilo halina mamlaka ya kubatilisha maamuzi ya TFF na Kamati ya Utendaji Yanga ambao walifikia makubaliano ya kujaza nafasi za viongozi Yanga ambazo hazina viongozi.
Akilimali amesema Yanga na TFF kwa pamoja walifikia mwafaka wa kumaliza kila kitu na kilichokuwa kimebakia ni kujaza nafasi sita pekee ikiwemo ya aliyekuwa Mwenyekiti wao, Yusuf Manji.
Kutokana na malalamiko hayo, imeelezwa pia Akilimali amewataka TAKUKURU kufuatilia barua iliyosomwa na Mkuchika juzi akieleza kuwa na wasiwasi nayo inawezekana kukawa na namna.
Mumbe Akilimali ameitaka taasisi hiyo kuifuatilia barua hiyo ili kuweza kujipatia uhakika zaidi kwani haamini kama Manji ameituma na ikiwezekana kuna watu wanatumika ndani ya klabu.