Kuelekea mchezo wa ligi kuu Tanzania bara kati ya Mtibwa Sugar dhidi ya Simba, kocha msaidizi wa ‘Wekundu wa Msimbazi’ Masoud Djuma amesema wanahitaji mambo mawili kutoka kwa mashabiki wao, sapoti na dua mambo mengine watamaliza wenyewe uwanjani.
Masoud amesema wanaiheshimu Mtibwa kwa sababu ni timu inayofanya vizuri kwa sasa kwenye ligi lakini mchezo wa raundi ya kwanza Simba iliponea chupuchupu.
“Tuna hitaji mambo mawili tu kutoka kwa wana simba sapoti na dua, mengine tutapambana sisi uwanjani”-Masoud Djuma.
“Tunaiheshimu Mtibwa ipo vizuri wakati huu kuna timu ambazo zinafanya vibaya lakini wao wapo vizuri.”
“Tukitazama mechi iliyopita tuliyocheza nao nyumbani, tuliponea chupuchupu japokuwa sisi wengine tulikuwa hatujafika. Tunawapa heshima zote lakini tutakuwa tunapambana kupata pointi tatu kwa hiyo tunahitaji kushinda.”
Mechi ya mzunguko wa kwanza kati ya Simba dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa uwanja wa Uhuru ilimalizika kwa sare ya kufungana 1-1, Simba wakisawazisha goli dakika za nyongeza kwa mpira wa adhabu ndogo uliopigwa na Emanuel Okwi.