Waziri wa Afya Zanzibar Mhe.Mahmoud Thabit Kombo katikati akionesha Cheti cha Ubora wa Huduma za Kiwango cha Kimataifa cha ISO 9001:2015 katika hafla iliyofanyika Ofisi za ZFDA Mombasa mjini Zanzibar
Waziri wa Afya Mahmoud Thabit Kombo katikati akizungumza mara baada ya kupokea Cheti
cha mfumo wa uhakiki ubora wa huduma cha kiwango cha kimataifa cha ISO
9001:2015 katika hafla iliyofanyika Ofisi za ZFDA Mombasa mjini Zanzibar
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar 15.02.2018
Wakala
wa Chakula na Dawa Zanzibar ZFDA umekabidhiwa rasmi Cheti cha mfumo wa
uhakiki ubora wa huduma cha kiwango cha kimataifa cha ISO 9001:2015.
Cheti
hicho cha ubora ni kielelezo cha taasisi ya ZFDA juu ya kusimamia
misingi imara ya kuhakiki ubora wa huduma katika kiwango cha kimataifa.
Akizungumza
mara baada ya kukabidhiwa Cheti hicho Waziri wa Afya wa Zanzibar
Mahmoud Thabit Kombo amesema mafanikio hayo ni matokeo ya utekelezaji wa
vitendo wa azma ya serikali inayoongozwa na Dkt. Ali Mohamed Shein
katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za afya hususan
upatikanaji chakula, dawa na Vifaa tiba.
Amesema
kunahitajika ubunifu na jitihada za makusudi za kila mfanyakazi wa ZFDA
kuhakikisha Chakula, Dawa, Vipodozi na Vifaa tiba ni bora na salama kwa
afya za wananchi.
Amefahamisha kuwa mafanikio hayo yaliyopatikana yawe chachu ya kuongeza ufanisi kiutendaji ili kufikia dira iliyowekwa.
“Mkifikia
dira dira hiyo itakuwa mmetekeleza kikamilifu jukumu mllopewa na
Serikali la kulinda afya ya jamii.Serikali inaaamini mnao uwezo wa kuwa
taasisi bora ya udhibiti Afrika na Duniani kwani hakuna kizuizi cha
kufikia dira hiyo” Alisema Waziri Kombo.
Aliitaka
menejimenti ya ZFDA kuimarisha udhibiti wa uingizaji wa Chakula, Dawa
na Vipodozi nchini kiholela ili kulinda afya za Wazanzibari.
“Ndugu
wafanyakazi mna jukumu kubwa sana kwa Wananchi wetu na mbele ya Mungu
maana mtakaporuhusu uingizwaji wa bidhaa duni zenye madhara mtahatarisha
afya za Wananchi na kesho mbele ya haki Mungu mutaulizwa” aliwanasihi
Waziri Kombo.
Kwa
upande wake Mwakilishi wa Kampuni ya ACM Ltd iliyokabidhi cheti hicho
Nyasha Mupukuta alisema haikuwa kazi rahisi kwa Taasisi hiyo kupatiwa
Cheti hicho cha ubora.
Alisema
kulipita ukaguzi wa kutosha na wa muda mrefu kabla ya Cheti hicho
kutolewa na hivyo kuendelea kuipongeza ZFDA kwa kazi kubwa
waliyoionesha.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ZFDA Burhani Othman Simai wakati
akielezea sababu zilizopeleka kupatiwa ZFDA kupatiwa Cheti hicho ni
pamoja na kuwepo kwa sera na miongozo ya ubora, mkataba huduma kwa
wateja, kanuni za maadili za wafanyakazi (code of Conduct), wafanyakazi
kusaini fomu za conflict of interest or competing interest na taratibu
sanifu za utendaji kazi (SOP).
Sababu
nyingine ni ufanyaji wa tathmini ya mteja kuridhika huduma zinazotolewa
(customer satisfication survey) na kuainisha majukumu ya kazi kwa kila
mfanyakazi (Job Description).
Hafla ya kupokea cheti hicho cha mfumo
wa uhakiki ubora wa huduma cha kiwango cha kimataifa cha ISO 9001:2015
zilifanyika katika Ofisi ya ZFDA Mombasa mjini Zanzibar na kuhudhuriwa
na Wakurugenzi mbalimbali na Mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Zanzibar
Andy Michel.