Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wakifuatilia uwasilishwaji wa muhtasari
wa Ripoti ya Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum ya Baraza
la Wawakilishi Zanzibar uliosomwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Machano
Othman Said, hayupo pichani
Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Katiba, Sheria,Utumishi wa Umma na Utawala Bora
Haroun Ali Suleiman kushoto akizungumza na Viongozi wa Ofisi ya Mufti
Zanzibar nje ya ukumbi wa Baraza la Wawakilishi mara baada ya kusomwa
muhtasari wa Ripoti ya Kamati ya Sheria, Utawala Bora na Idara Maalum ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Mwenyekiti
wa Kamati ya Sheria, Utawala Bora Idara za Maalum ya Baraza la
Wawakilishi Machano Othman Said katikati akizungumza na baadhi ya
Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi mara baada ya kuwasilisha Muhtasari wa
Ripoti ya Kamati hiyo kwa mwaka 2017-2018.
Na Miza Kona Maelezo – Zanzibar 15/ 02/2018
Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar imeombwa kuongeza nguvu za kuwapatia wataalamu na
vitendea kazi Manispaa ya Magharibi ‘A’ na ‘B’ ili ziweze kupiga hatua
kubwa kimaendeleo na ukusanyaji wa mapato.
Hayo
yamesemwa huko Baraza la Wawakilishi Chukwani na Mwenyekiti wa Kamati
ya Sheria, Utawala Bora Idara za Maalum ya Baraza la Wawakilishi Mhe
Machano Othman Said wakati akiwasilisha Muhtasari wa Ripoti ya Kamati
hiyo kwa mwaka 2017-2018.
Alisema Kamati imeridhishwa
na ukusanyaji wa mapato wa Manispaa hizo ambazo ni mpya hivyo ipo haja
kwa serikali kuongeza juhudi zitakazosaidia kuleta mabadilko ya
maendeleo na kuongezo kipato nchini.
“Kamati
yetu kwa kiasi kikubwa imeridhishwa na ukusanyaji wa mapato wa Manispaa
hizi ambazo ni mpya na tunaomba wazidi kuongeza juhudi”, alieleza Mhe
Machano Othman.
Alieleza
kuwa Manispaa hizo zinafanya kazi kubwa japo kuwa zinakabliwa na
changamoto nyingi ikiwemo ongezeko kubwa la idadi ya wakaazi na
wahamiaji kutoka maeneo tofauti.
Changamoto
zingine ni ubovu wa miundombinu ya barabara, upungufu wa huduma za
kijamii ikiwemo maji safi na salama, umeme na Skuli za msingi katika
maeneo ya Manispaa hizo.
Aidha Mwenyekiti huyo alifahamisha kuwa, kuwepo kwa bandari zisizo rasmi katika maeneo
ya Uzi na Bungi huchangia vitendo vya kihalifu ikiwemo kuvamiwa Wageni
na uingizwaji wa bidhaa za magendo na zisizokuwa na Viwango vya ubora.
Hata
hivyo Mwenyekiti wa Kamati hiyo alieleza kuwa mbali na changamoto
zinazojitokeza katika Manispaa hizo maendeleo ya manispaa hizo
yanaonekana.
Kuhusu
Afisi ya Mufti, Kamati hiyo imeishauri Wizara ya Katiba na Sheria
kuwapatia jenereta kwa ajili ya kukabiliana na tatizo la nishati ya
umeme katika Afisi hiyo.
Kamati
hiyo imeishauri pia Afisi ya Mufti Zanzibar kufuatilia kiundani
utendaji wa Afisi ya Mufti Pemba ili kuhakikisha kuwa wanaboresha
utendaji wao katika majukumu yao ya msingi.
Wakichangia
Ripoti hiyo baadhi ya Wajumbe wa Baraza hilo wamesema tatizo la rushwa
bado linaendelea kuwepo na kupelekea baadhi ya kesi kukwama
katika manipaa hizo.
Hivyo
wameziomba taasisi husika kupambana kikamilifu na tatizo la Rushwa
ambalo linaendelea kuwaathiri Wananchi wengi katika harakati za maisha
yao.