Jeshi la Polisi Mkoa wa Kusini Unguja limewaachia kwa dhamana wanaume 10 waliokuwa wakishikiliwa katika kituo cha Polisi Chwaka Mkoa wa Kusini Unguja kwa tuhuma za kujihusisha na mapenzi ya jinsia moja.
Akithibitisha kuachiwa kwa watuhumiwa hao Kamanda wa Polisi Kusini Unguja Suleiman Hassan amesema awali walipokea taarifa kuwa Wanaume hao wapo katika Fukwe ya Pongwe wakifanya vitendo vya kiuhalifu lakini baada ya kuwakamata na kufanya nao mahojiano wamebaini kuwa watu hao si wahalifu hivyo wamewaachia kwa dhamana na pindi wakiwahitaji watarudi tena Kituoni kwa maelezo zaidi.
Kamanda Suleiman Hassan ametoa taarifa hiyo wakati akizungumza na Zanzibar24 na alipoulizwa juu ya vijana hao kuhusishwa na madai ya Ushoga alisema “Kwasababu hatukuwakuta katika hali ile ya Ushoga kama inavyozungumzwa na hatukuwa na ushahidi hivyo baada ya mahojiano kituo cha Polisi Chwaka tumewakuta bila hatia tumewaachia “
Taarifa ya kukamatwa kwa wanaume hao iliyotolewa awali na Shirika la kutetea Haki za Binaadamu la Amnesty International limeripoti kuwa wanaume hao 10 wamekamatwa Jumamosi iliyopita katika fukwe ya Pongwe walipokuwa katika harusi ya mashoga. Wengine sita walifanikiwa kuwatoroka polisi.
“Polisi walifika eneo la tukio baada kupewa taarifa na wananchi kuwa kuna harusi ya mashoga inaendelea…Watu hao wanashikiliwa katika kituo cha polisi Chwaka na mpaka sasa hakuna mashtaka yoyote yaliyofunguliwa,” ilisema ripoti ya Amnesty siku chache zilizopita.
Hata hivyo Kamanda amemalizia kwa kusema iwapo lolote litatokea jeshi la Polisi litawaita tena wanaume hao kwa mahojiano zaidi.