MZUNGUKO
wa 15 wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara unatarajiwa kuendelea leo
kwa mechi nne, lakini kubwa zaidi ni kati ya Azam FC na Yanga SC Uwanja
wa Azam Complexm, Chamazi, Dar es Salaam kuanzia Saa 10:00 jioni.
Mechi nyingine za leo Mwadui FC watakuwa wenyeji wa Njombe Mji FC Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, Mbeya City watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na Kagera Sugar wataialika Lipuli FC Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Yanga wanaifuata Azam FC kinyonge leo bila wachezaji wake saba ambao ni mabeki Pato Ngonyani, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, viungo Pius Buswita, Thabani Kamusoko na washambuliaji Amissi Tambwe, Yohana Nkomola na Donald Ngoma.
Kuna pia Yanga ikaendelea kumkosa kocha wake mkuu, Mzambia George Lwandamina ambaye hadi jana jioni alikuwa bado hajapatiwa kibali cha kufanya kazi nchini, ingawa uongozi ulisema ulikuwa unakaribia kupatiwa.
Wakati huo huo; Kocha Msaidizi wa Yanga, Nsajigwa Shadrack Mwandemele hatakuwepo leo kwa sababu amefiwa na shemeji yake, hivyo amekwenda kuzika. Ni Kocha wa mazoezi ya viungo pekee, Mzambia mwingine, Noel Mwandila ambaye yuko tayari kuingoza timu kwa mchezo wa kesho hadi sasa.
Pamoja na hayo, wapinzani wao, Azam FC walianza kuonyesha mchecheto juzi kufuatia kuandika barua kwenda Bodi ya Ligi Tanzania Bara (TPLB) kuelezea kutokuwa na imani na mwamuzi Israel Nkongo aliyepangwa kuchezesha mchezo huo.
Barua hiyo ilizidi kueleza kuwa moja ya sababu nyingine ya kumlalamikia mwamuzi huyo na kukosa imani naye, ni kitendo chake cha kuzua utata mkubwa kwenye mchezo aliochezesha mkoani Mbeya wiki moja iliyopita kati ya Tanzania Prisons na Mbeya City kutokana na uamuzi wake.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohamed, aliyeandika barua hiyo na kutuma nakala kwa Kamati ya Waamuzi, TFF na Yanga, ameweka wazi kuwa kwa kuzingatia uzito wa mchezo huo wameiomba bodi hiyo kubadilisha mwamuzi kwa kumpanga mwingine.
Aidha, katika barua hiyo, Mohamed ameongeza kuwa kutokana na timu zote mbili kutoka katika mkoa wa Dar es Salaam, ameiomba bodi hiyo kumpanga mwamuzi ambaye atatoka nje ya mkoa huo.
Mbali na Nkongo kupangwa kuchezesha mchezo huo, waamuzi wengine waliopangwa kushirikiana naye ni Josephat Bulali atakayekuwa mwamuzi msaidizi namba moja, msaidizi namba mbili atakuwa Soud Lila, mwamuzi wa akiba ni Elly Sasii huku Omar Abdulkadir akiwa Kamishna wa mchezo huo, wote wakitoka Dar es Salaam.
Duru la kwanza la Ligi Kuu litakamilishwa Jumapili kwa mechi mbili, vinara Simba SC wakimenyana na Maji Maji FC ya Songea Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam na Singida United watakuwa wenyeji wa Tanzania Prisons Uwanja wa Namfua mkoani Singida.
Ikumbukwe Simba SC, inagongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 32, ikifuatiwa na Azam FC pointi 30 na Yanga, ambao ndio mabingwa watetezi, wanafuatia kwa mbali katika nafasi ya tatu kwa pointi zao 25.