Rais wa Simba Evans Aveva hali yake sio nzuri na anaendelea kutibiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete.
Jana Aveva alishindwa kufika mahakamani kwa mara ya saba lakini ndugu yake akaliambia Championi, hali yake si nzuri.
“Hali yake si nzuri, anaumwa sana kwa kweli na sisi tunajisikia vibaya lakini ni kipindi cha mapito. Unajua bado ana kesi lakini kweli Aveva anaumwa sana na hata ukimuona, anaumiza sana moyo,” alisema.
Aveva amekuwa akizidi kupungua kutokana na kuugua mfululizo siku chache baada ya kuingia mahabusu akituhumiwa katika kesi ya utakatishaji fedha.
Jana, Aveva ameshindwa kuhudhuria tena mahakamani katika kesi yake ya utakatishaji fedha inayomkabili ikiwa ni mara ya saba mfululizo kutokana na kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kufuatia hali yake ya kiafya kutokuwa nzuri.
Aveva anakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha kiasi cha dola 300,000 za Kimarekani, akiwa na makamu wake wa rais, Geofrey Nyange ‘Kaburu’.
Katika kesi hiyo ambayo itakuwa ikisikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Makahama ya Kisutu, Thomas Simba, badala ya Victoria Nongwa ambapo wakili wa Takukuru, Nassor Katuga ameiambia mahakama hiyo kwamba kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa lakini wameshakamilisha upelelezi, hivyo wapo tayari kuendelea kwa hatua ya kuanza kusikilizwa.
Katuga alisema kuwa wamepokea taarifa kuwa mshitakiwa namba moja (Aveva) ameshindwa kufika mahakamani kwa kuwa anaumwa na amelazwa Muhimbili, badala yake yupo Kaburu peke yake ambaye ni mshitakiwa namba mbili.
Kwa upande wa hakimu Simba, alisema kuwa ni vyema kufuatilia hali yake kwa kuwa kesi ipo tayari kusikilizwa ili iweze kuendana na muda kutokana na kuwa ni ya muda mrefu ambapo amepanga kuanza kusikilizwa Aprili 5, mwaka huu.