Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokuwa na mazungumzo na ujumbe kutoka Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” kutoka nchini China ambayo imedhamiria kuekeza katika kiwanda cha Makonyo, kilichopo Wawi Pemba kwa kushirikiana na Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC).
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein aliihakikishia Kampuni hiyo kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itatoa ushirikiano wake mkubwa kupitia Wizara yake ya Biashara na Viwanda pamoja na Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC).
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuipongeza Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” chini ya Mwenyekiti wake Zhou Junxue kwa kusaini Makubaliano ya Awali kati ya Kampuni hiyo na Shirika la (ZSTC
Aidha, Dk. Shein aliueleza ujumbe wa Kampuni hiyo kuwa Kiwanda cha Makonyo kilichopo Wawi ni cha muda mrefu ambacho kimekuwa kikizalisha mafuta ya aina mbali mbali hivyo, ushirikiano wa pamoja katika uzalishaji kiwandani hapo kutasaidia kuinua ubora wa kiwanda sambamba na kuongeza pato la Taifa na soko la ajira.
Alieleza kuwa uwamuzi wa Kampuni hiyo ni mzuri na umekuja katika wakati muwafaka ambapo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imo katika kutekeleza Sera ya Uchumi wa Viwanda, hivyo hatua hiyo itakuwa chachu katika kufikia malengo yaliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar imejaaliwa kuwa na viungo vya vyakula vya aina nyingi ambavyo miongoni mwao vimekuwa vikitoa mafuta bora ambayo yamekuwa ni bidhaa muhimu iliyoingia katika soko la ndani na nje ya Tanzania yakiwemo mafuta ya makonyo, mafuta ya karafuu na mafuta ya mikaratusi.
Hivyo, Dk. Shein aliongeza kuwa kuanza kwa uwekezaji huo kutazidi kuitangaza Zanzibar na kuwa kiwanda cha pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kinachozalisha bidhaa hizo za mafuta.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza haja ya Kampuni hiyo kushirikiana na ZSTC katika kutekeleza makubaliano hayo yaliotiwa saini hapo jana ikiwa ni pamoja na kuongeza zaidi uzalishaji huku akisisitiza suala zima la ufanyaji utafiti katika kilimo cha mazao hayo yanazotoa mafuta.
Aidha, Dk. Shein alisisitiza suala la mafunzo ambalo litasaidia sana kuendesha kiwanda hicho pamoja na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za aina mbali mbali za mafuta ya viungo kutoka katika kiwanda hicho cha Makonyo Wawi jambo ambalo pia, litaongeza soko la ajira hapa nchini.
Nae Mwenyekiti wa Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” ya China, Zhou Junxue alimpongeza Rais Dk. Shein kwa juhudi zake katika kuimarisha uchumi wa Zanzibar kwa kupitia sekta ya viwanda vikiwemo viwanda vidogo na vya kati.
Mwenyekiti wa Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” alimueleza Rais Dk. Shein mikakati iliyowekwa na Kampuni yake katika kuhakikisha makubaliano waliyosaini yanatekelezwa kwa lengo la kuleta manufaa kwa pande zote mbili.
Junxue alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa Kampuni yake itatoa mashirikiano makubwa kwa Serikali kupitia Shirika lake la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) katika kuhakikisha kiwanda hicho kinatoa mafuta yalio bora sambamba na kuongeza uzalishaji wa bidhaa zitakazozalishwa katika kiwanda hicho cha Wawi.
Kampuni ya “Kunshan Asia Aroma Cooperation Limited” ya nchini China ambayo ndio mnunuzi mkubwa wa mafuta ya viungo vya Zanzibar tokea Julai mwaka 2017, ilitiliana saini Makubaliano ya Awali na Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) katika kuendesha mradi ndani ya miaka kumi utaohusisha uimarishaji wa utendaji na utaalamu katika kiwanda cha Makonyo Wawi.
Jambo jengine ni uendelezaji wa mazao ya karafuu na mikaratusi ili kuongeza uzalishaji kutoka tani 60 zinazozalishwa hivi sasa hadi kufikia tani 2,000,
ubadilishanaji uzoefu kati ya watendaji wa taasisi hizo, upatikanaji wa mafunzo, mbinu na upatikanaji mbegu bora za mikaratusi ni miongoni mwa makubaliano hayo.