Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, (UN), Antonio Guterres amemteua Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania, Mohammed Chande Othman kuongoza jopo la uchunguzi wa kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa UN, Dag Hammarskjöld.
Hammarskjold aliyekuwa katibu mkuu wa pili wa UN alifariki dunia Septemba 18 1961 katika ajali ya ndege iliyotokea huko Ndola, Zambia, wakati akiwa katika safari ya kikazi ya kuhamasisha amani Zaire, kwa sasa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Uteuzi wa Jaji Othman huo ni kwa mujibu wa azimio namba 72/252, la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na uteuzi huo unajumuisha jopo la wajumbe aliokuwa nao awali.
Uteuzi huo unatokana na ripoti iliyowasilishwa na Baraza Kuu la UN ambalo lilibaini kuwa pamoja na mambo mengine, sababu kuu ya kuanguka kwa ndege hiyo ni shambulizi la nje au vitisho vilivyosababisha ndege hiyo ianguke.
Taarifa ya UN, imewataka nchi wanachama kumpa ushirikiano Jaji Chande wakati akitekeleza majukumu yake, ikiwamo kumpa taarifa zinazoweza kumsaidia katika uchunguzi wake.