Katibu Tawala wa Wilaya ya Chake Chake Pemba, Abdalla Rashid Ali, akimkabidhi zawadi mtoto Yatima baada ya kukabidhiwa na Mkurugenzi wa Taasisi ya Samael Academy, Sheikh Nassir Bin Said Al-Rawahy, huko Gombani Pemba.
PICHA NA OMAR MJAKA KUTOKA TAASISI YA SAMAEL ACADEMY.
Mkurugenzi wa taasisi ya Samael Academy, Sheikh , Nassir Bin Said Al-Rawahy, akibadilishana mawazo na Katibu Tawala wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, katika hafla ya utowaji wa Zawadi kwa watoto Mayatima , ilioandaliwa na taasisi hiyo.
PICHA NA OMAR MJAKA KUTOKA TAASISI YA SAMAEL ACADEMY.
Na Aziz Simai, Pemba
Serikali ya Mkoa wa Kusini Pemba, imeahidi kushirikiana na taasisi ya Samael Academy iliyoko Gombani Chake-Chake Pemba, ili iweze kufikia malengo ya kutoa elimu bora kwa jamii.
Akizungumza katika hafla fupi ya utoaji sadaka kwa watoto yatima kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Katibu Tawala Wilaya ya Chake-Chake Pemba, Abdalla Rashid Ali, alisema malengo ya taasisi hiyo ni faraja kwa Mkoa huo katika utoaji wa elimu ya fani mbali mbali ikiwemo elimu ya ufundi kwa vijana.
Katibu Tawala huyo ,alieleza kuwa Serikali ya Mkoa huo pamoja na Wilaya zitajitahidi kushirikiana ili kuona changamoto zilizoikabili Taasisi hiyo yaSamael academy inapatiwa ufumbuvi wa haraka ili shughuli za Taasisi ziweze kuanza mara moja.
Akizungumza malengo makuu ya Taasisi hiyo , Mkurugenzi wa Taasisi hiyo ya Samael academy, Sheikh Nassir Said Al-Rawahy alisema wamekusudia kufundisha masomo mbali mbali yakiwemo ya biashara na ufundi lakini shuhuli hizo zimechelewa kuanza kutokana na kuchelewa kupata usajili kutoka baraza la mitihani Tanzania (NACTE).
Sheikh Nassir, alifahamisha mbali na hilo Taasisi hiyo inaendelea na shughuli zake nyengine ikiwemo ujenzi wa miskiti, uchimbaji wa visima, kutoa sadaka kwa mayatima na kusaidia shughuli za madrasa za Qur-an.
Katika hafla hiyo jumla ya wanafunzi 100 mayatima, walipatiwa sadaka ya fedha taslim pamoja na zawadi nyengine mbali mbali.