Kutokana na safu ya ushambuliaji ya Kagera Sugar kushindwa kufunga magoli ya kutosha kocha wa timu hiyo Meck Maxime amemkumbuka mfungaji wao wa msimu uliopita Mbaraka Yusuph ambaye alisajiliwa Azam kwamba huenda angewasaidia katika kipindi hiki.
Katika mchezo wao wa ligi Machi 9, 2018 dhidi ya Yanga ambao walipoteza kwa kufungwa 3-0, Kagera Sugar ilitengeneza nafasi za kufunga lakini hawakuweza kufunga goli hata moja.
“Mwaka jana tulikuwa na Mbaraka ambaye analijua goli lakini mwaka huu tunakuja Mbara hayupo, mtu ambaye tulishamtengeneza anakupa kitu mwaka unaofuata tena akuongezee hayupo anakuja mwingine inabidi umtengeze lakini hizi timu kubwa wenzetu wana watu ambao wanaamua matokeo, hata kama muda wote hayupo uwanjani lakini akipata nafasi moja hiyohiyo anaitumia.”
“Sisi tumecheza mpira lakini matokeo tumekosa lakini wenzetu wametumia nafasi wamepata matokeo ndiyo mpira unavyokuwa.”
Maxime bado anaamini timu yake itabaki kwenye ligi licha ya kuwa kwenye nafasi za chini kwa sasa, amesema katika mechi tisa walizobakiza kabla ya ligi kumalizika watafanya kila kitu kuhakikisha wanainusuru timu yao isishuke daraja.
“Bado tunapambana kwa sababu bado mechi tisa bado hatujakata tama tunaamini hatuwezi kushuka na tutasogea juu.”
Kagera sugar ipo nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi baada ya kucheza mechi 21.