NA SALEH ALLY
KUNA jambo tunaweza kujifunza na mwisho kujua faida ya kuwepo kwa Azam FC katika mchezo wa soka nchini, kwamba ni kubwa sana.
Nimeanza
kuufuatilia mpira wa Tanzania Bara wakati ule kukiwa na wapinzani kama
akina Sigara, Nyota Nyekundu, Mecco na Tukuyu Stars za Mbeya, CDA ya
Dodoma, Biashara Shinyanga, Pamba ya Mwanza na nyingine.
Kama nitazungumzia sana timu hizo, huenda nitawapiga chenga watu wengi sana wa kizazi cha mpira wa sasa.
Hata
mimi kuna mengi sikumbuki sana ingawa nilibahatika kuwashuhudia
wachezaji mahiri wa zamani kama Celestine Sikinde Mbunga wa Majimaji.
Baadaye kizazi ambacho nimekulia mimi cha akina Edibily Lunyamila.
Wakati
huo, Yanga na Simba walikuwa na upinzani mkubwa sana ndiyo maana uliona
timu kama Coastal, African Sports, Majimaji na nyingine ziliweza kubeba
ubingwa mbele ya wakongwe Yanga na Simba.
Baadaye,
mambo yalibadilika baada ya kuanza kudorora kwa timu hizo na ushindani
ukashuka kwa kiasi kikubwa. Simba na Yanga wakawa wanafanya wanavyotaka
wao na si vingine.
Muda
umesonga zikiwa na ufalme huo, lakini ndani ya miaka sita utaona kuna
mabadiliko makubwa ambayo yameingizwa na Azam FC ambao ndani ya miaka
minne wamechukua ubingwa mara moja.
Ushindani
wao wamevuruga ule “upacha” wa Yanga na Simba, kuwa kama leo si huyu,
yuko yule na ni walewale. Unakumbuka timu kama zile nilizokutajia
ziliwahi kuingia na kuchukua ubingwa mbele ya Yanga na Simba.
Simba
wamekuwa hawashiriki michuano ya kimataifa kutokana na uwepo wa Azam FC
na hii inaongeza ushindani na wingi wa mechi kubwa.
Takribani
miaka 10, Simba dhidi ya Yanga ndiyo imekuwa mechi kubwa inayosubiriwa,
hadi ilipoibuka Azam FC na utaona imebadilisha mambo kwa siku za hivi
karibuni na kurejesha ule ushindani wa kipindi kile Coastal, African
Sports, Sigara au Pilsner zikiwa katika kiwango chake.
Mfano
mzuri ni mechi mbili za hivi karibuni, Azam FC ilipoikaribisha Yanga
kwenye Uwanja wa Azam Complex, ikapoteza kwa mabao 2-1, ikakaribishwa na
Simba Uwanja wa Taifa, pia ikapoteza kwa bao 1-0.
Pamoja
na kupoteza kwa Azam FC, mechi hizo zinaweza kuwa mfano au kitu cha
kuzungumzia katika mpira wa Tanzania kwa kuwa ushindani ulikuwa mkubwa
na mpira ulichezwa kweli.
Tumeona
mechi kadhaa badala ya soka kupewa kipaumbele, kunakuwa na tafrani na
mambo yasiyo na msingi. Lakini mechi hizo mbili, tumeona Azam FC
ikipambana kweli na wakongwe hao na ilikuwa mechi ambayo hauwezi kujua
nani atashinda.
Mechi
dhidi ya Yanga ilikuwa ni ile ambayo hauamini kama dakika 90 zitaisha
na sare au mmoja kushinda. Lakini ile dhidi ya Simba, nayo ilikuwa
vigumu kuamini Simba watashinda au ni sare hadi usikie kipenga cha
mwamuzi.
Mechi
za Ligi Kuu Bara, zinapaswa kuwa na ushindani wa namna ile na hakika
kweli Azam FC, imeongeza utamu wa Ligi Kuu Bara kutokana na ushindani
wake.
Angalia
Azam FC, leo imetengeneza mechi nyingine nne za Ligi Kuu Bara ambazo
zinaweza kuitwa “Big Match” badala ya watu kuendelea kusubiri mechi
mbili tu katika msimu ambazo zinaitwa “Big Match”. Tena katika mechi
hizo kubwa, unashuhudia soka safi na la ushindani, jambo ambalo ni bora
zaidi kwa nembo ya maendeleo ya mpira wa Tanzania.
Hakuwezi
kuwa na ligi bora kama hakuna ushindani sahihi wenye vipimo bora.
Mwendo wa Azam unachangia hofu ya kusaka maendeleo kwa wakongwe Yanga na
Simba na hofu ya maendeleo ni bora katika kusaidia kupatikana kwa
mafanikio.
Mechi
hizo dhidi ya Azam FC na wakongwe ni ladha zaidi na maendeleo zaidi.
Huenda timu nyingine nazo zinaweza kuamka na kuongeza ubunifu ili
kujenga ubora unaoweza kuzitikisa Yanga na Simba ili kusaidia kuongesha
ushindani na maendeleo pia.