Mkuu
wa Simba Mfaransa, Pierre Lechantre anatarajiwa kukaa kwa mara kwanza
kwenye benchi la timu hiyo kesho Jumapili wakati watakapoivaa Majimaji
ya Ruvuma, lakini amechimbwa mkwara na straika wa wapinzani wao hao.
Jerry
Tegete ambaye ni straika wa Majimaji FC inayodhaminiwa na Kampuni ya
Kubashiri Matokeo ya Sokabet, amedai anataka kuvuruga ‘fungate’ la Simba
na kocha huyo ambaye ameanza kazi Jumanne wiki hii.
Majimaji
itaivaa Simba katika mechi ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa kwenye Uwanja
wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo awali Majimaji ilitoka sare ya bao
1-1 na Yanga mkoani Ruvuma.
Kocha
wa Simba alitua nchini wiki iliyopita na kusaini mkataba wa miezi sita
wa kuifundisha timu hiyo akiwa pamoja na msaidizi wake raia wa Tunisia,
Mohammed Aimen.
Tegete
alisema ujio wa kocha huyo mpya hauwafanyi wao waogope na kupata
matokeo mabaya, kwani wataingia uwanjani kwa ajili ya ushindi pekee.
“Kama
unavyojua ligi inaelekea katika mzunguko wa pili, hivyo ni lazima
tushinde michezo yote iliyokuwepo mbele yetu ili tujiweke katika nafasi
nzuri katika msimamo,” alisema Tegete.
Alisema
walianza na sare mbili kutoka kwa timu kubwa zenye upinzani mkubwa
ambazo ni Azam FC na baadaye Singida United, hivyo wanaofuata ni Simba.
“Tunajua
Simba wameleta kocha mpya Mfaransa, lakini hiyo haitufanyi sisi
kuwaogopa, kwani tuna timu imara itakayoleta ushindani, tumetoka sare na
Azam na Singida United ambazo pia zina makocha Wazungu, hivyo
tunakwenda kucheza na Simba tukifuata matokeo mazuri ya ushindi na siyo
kitu kingine,” alitamba Tegete.