Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia Mkutano wa Tano wa Jumuiya ya Wataalamu wa Figo Tanzania, wakati wa ufunguzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Karume Hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini Zanzibar.23/11/2018.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amesema
Serikali inaendeleza sera na dhamira ya Mapinduzi
matukufu ya 1964, kwa kutoa huduma bure za
matibabu kwa wananchi wa Zanzibar bila ubaguzi.
Alisema hatua hiyo inakwenda sambamba na sera na Ilani ya
Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 – 2020.
Dk. Shein amesema hayo leo, alipofungua mkutano wa tano
(5)wa Chama cha Wataalam wa Figo Tanzania (NESOT),
uliofanyika katika Hoteli ya Zanzibar Beach Resort, nje
kidogo ya Mji wa Zanzibar.
Mkutano huo siku tatu unaowashirikisha viongozi,
wataalam,madaktari,wauguzi, na wadau mbali mbali kutoka ndani na nje ya nchi, unaambatana na kauli mbiu “Uimarishaji wa matibabu ya figo katika maeneo yenye changamoto za rasilimali tiba”.
Dk. Shein alisema pamoja na kuwepo ongezeko kubwa la
watu hapa nchini, sambamba na kupanda kwa gharama za
matibabu ya magonjwa mbali mbali ikiwemo figo, serikali
itaendelea kusimamia sera hiyo ikiwa ni hatua ya kuyaenzi
Mapinduzi hayo.
Alisema kwa mnasaba huo, katika bajeti ya mwaka wa fedha
wa 2018/2019, Serikali imeongeza bajeti ya dawa hadi
kufikia shilingi Bilioni 12.7 (sawa na asilimia 81.43) kutoka shilingi Bilioni 7 zilizotengwa katika mwaka 2017/2018.
“Katika juhudi za kuimarisha huduma bora za Afya,
tumeimarisha bajeti ya Wizara Afya kwa mwaka 2018/2019,
kwa asilimia 81.43, hatua hii ni utekelezaji wa ahadi ya
kuwapatia matibabu bure wananchi wote’, alisema.
Alieleza kuwa Tanzania ina wagonjwa wengi wa ugonjwa wa
figo na kubainisha changamoto kadhaa zilizopo katika
kuukabili ugonjwa huo, ikiwemo upungufu wa nyenzo na
rasilimali.
Alisema juhudi za kukabiliana na ugonjwa huo zilianza
kipindi kirefu na kuwapongeza waanzilishi wake, akiwemo
Dk. Mohamed Jidawi, Dk. Jamalla Adam na marehemu Dk.
Malik Abdalla, ambapo kwa ushirikiano na washirika mbali
mbali wa Maendeleo na Chuo Kikuu cha Haukland cha
nchini Norway, juhudi hizo zimeanza kuzaa matunda.
Alisema Serikali itaendelea na juhudi za kuimarisha
huduma na kuongeza wataalamu wabobezi katika tiba ya magonjwa ya figo nchini, ili kukabailiana vilivyo na ugonjwa huo hatari.
Aidha, alipongeza juhudi zinazoendelea kuchukuiliwa na
NESOT katika kuwashajiisha madaktari wake katika suala la
kufanya utafiti na kubainisha kuwa tafiti hizo zitasaidia
kupatikana ufumbuzi wa matatizo mengi kuhusiana na
ugonjwa huo.
Dk. Shein aliagiza kuwepo programu maalum, itakayokuwa
na dhima ya kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa
kuchukuwa tahadhari ili kupunguza ukubwa wa tatizo la
‘mshtuko wa ghafla wa figo’ (acute kidney injury), ambalo
alisema ni hatari sana kwa jamii.
Alikitaka chama hicho kuendelea kuishajiisha jamii, hususan
vijana kusoma taaluma ya fani ya tiba ya binadamu, ili
hatimae waweze kupata wanachama wengi zaidi.
Vile vile aliwataka wataalamu hao kutokuvunjika moyo
kutokana na changamoto mbali mbali wanazokabiliana
nazo, na badala yake waongeze juhudi na kufanya kazi kwa kutawaliwa na dhamira, kwa kigezo kuwa hakuna kinachoshindikana.
Katika hatua nyengine, Dk. Shein aliwataka wanafunzi
walioshiriki mkutano huo kuwa makini wakati wa
majadiliano, ili kuongeza uwelewa wao katika mambo mbali
mbali. ambapo darasani hawawezi kuyapata.
Nae, Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid Mohammed,
aliahidi Wizara yake kushughulikia uanzishaji wa kituo cha
tiba ya ugonjwa wa Figo kisiwani Pemba ili kupanua wigo wa
upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Aliwataka wanafunzi walioshiriki kongamano hilo kutumia
vyema fursa hiyo na kupokea utaalamu kutoka kwa
madaktari bingwa kutoka nchi mbali mbali duniani.
Aidha, aliwataka madaktari na wataalamu wa afya nchini,
kuongeza ushirikiano kati yao ili kuleta ufanisi katika
utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
”Kumekuwepo na matukio ya wagonjwa kufariki dunia, kwa
sababu tu daktari mmoja hataki ‘ku- share’ na mwenzake
kupata mawazo mapya ya tiba”, alisema Waziri Hamad.
Mapema, Katibu Mkuu wa Wizara Afya, Asha Ali Abdalla
alisema kuanzishwa kwa huduma ya tiba ya ugonjwa wa figo
nchini, kumetokana na serikali kutambua na kuthamini
mahitaji ya wanyonge katika upatikanaji wa huduma hiyo
inayohitaji gharama kubwa.
“Lengo ni kutanua wigo katika kuwafikia wananchi wengi
zaidi wenye mahitaji ya huduma hii’, alisema.
Alisema pamoja na juhudi kubwa zinazochukuliwa na
Serikali katika kukabiliana na ugonjwa huo, kumekuwepo
changamoto mbali mbali zinazojitokeza, ikiwemo uchache
wa wataalamu na ukosefu wa vifaa.
Aidha, Rais wa Chama cha wataalamu wa Figo Tanzania
(NESOT), Dk.Onesmo Kisanga, alisema inakadiriwa watu
wapatao 160, 000 wanakabiliwa na ugonjwa huo hapa
Zanzibar.
Alisema utafiti uliofanywa na Chama hicho umebaini kuwa
asilimia 6.8 ya Watanzania wanakabiliwa na ugonjwa huo,
wakiwa bado hawajajitambua.
Alibainisha kuwa pamoja na gharama kubwa za tiba ya
ugonjwa wa figo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
imefanikiwa kutoa tiba bure kwa wagonjwa wanaojitokeza
kufuata matibabu.
Alisema kwa kutambua ugumu na gharama za matibabu ya
ugonjwa huo, NESOT imejipanga kutoa elimu kwa jamii,
ikiwa ni hatua ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Aidha, alipongeza mafanikio makubwa yaliopatikana kwa
Tanzania kuwa na jumla ya vituo tisa (9) vya kusafishia
damu (dialysis).
Dk. Kisanga alisema Kongamano hilo lina dhima ya
kuimarisha huduma za matibabu ya Afya katika maeneo
yenye changamoto za ugonjwa huo.
“Dhima ya kongamano hili ni kuboresha na kuimarisha
matibabu ya figo katika maeneo yenye changamoto za
ugonjwa huu, tutajadili yaliotokea Zanzibar, Tanzania,
Afrika, India na dunia kwa jumla, lakini pia mafanikio na
changamoto zitajadiliwa’, alisema.
Viongozi mbali mbali walihudhuria kwenye mkutano huo,
akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif
Ali idd.