Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara Zanzibar, akifungua Mkutano wa Pili wa Baraza la Taifa la Biashara Zanzibar, katika ukumbi wa Ikulu Zanzibar.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein amesema kuwa kuanzishwa kwa Sheria namba 10 ya mwaka 2017 ya Baraza la Taifa la Biashara la Zanzibar (ZNBC) kutaimarisha sekta ya biashara na kukuza uchumi nchini.
Dk. Shein aliyasema hayo leo Ikulu mjini Zanzibar wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Baraza la Taifa la Biashara la Zanzibar (ZNBC) wa siku moja ambao pia, mbali ya mambo mengine ulijadili maandalizi ya Jukwaa la Tisa la Biashara la Zanzibar litakalofanyika Novemba 24, 2018.
Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein alieleza imani yake kubwa kuwa Sheria hiyo namba 10 ya mwaka 2017 italeta kasi kubwa katika kuimarisha ushirikiano kati ya sekta Binafsi na Serikali kwa lengo la kukuza uchumi wa Zanzibar.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa mkutano huo wa leo umejadili mambo ya msingi yenye mnasaba na Jukwaa la Tisa la Biashara la Zanzibar ambao utaweza kusaidia katika kulifanikisha Baraza la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZNBC) ili kufikia malengo iliyojiwekea.
Dk. Shein alisisitiza haja kwa wajumbe wa Baraza hilo kuhudhuria vikao ipasavyo kutokana na umuhimu mkubwa wa Baraza hilo kwani vikao hivyo huamua na kujadili mambo muhimu.
Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuandaliwa taratibu maalum za kuwasaidia vijana ili waweze kushiriki vyema katika uzalishaji wa bidhaa mbali mbali zikiwemo za kilimo, uvuvi, utalii na nyenginezo ambapo kwa upande wa Serikali alieleza hatua zinazochukuliwa ili kufanikisha hilo.
Alileza kuwa kuna haja ya sekta binafsi kushirikiana na sekta ya umma katika kuwasaidia vijana huku akisisitiza kuwa vikao hivyo vina umuhimu mkubwa katika kujenga muktadha mzuri wa malengo yaliokusudiwa.
Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuwaandaa vijana wa Zanzibar ili waweze kujijengea mazingira mazuri ya ajira kwa mashirikiano ya pamoja kati ya sekta Binafsi na Serikali.
Akitoa maelezo juu ya Sheria namba 10 ya 2017 ya Baraza la Taifa la Biashara la Zanzibar (ZNBC) Mohammed Khamis, Mwanasheria kutoka Wizara ya Biashara na Viwanda alisema kuwa kuwepo kwa Sheria hiyo kuna umuhimu mkubwa katika kuimarisha sekta ya biashara na uchumi hapa Zanzibar.
Alisema kuwa Sheria hiyo imeeleza mambo mengi ikiwa ni pamoja na muundo wa vyombo mbali mbali, likiwemo Baraza la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZNBC), malengo kadhaa pamoja na kazi mbali mbali za Baraza la Taifa la Zanzibar.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na kuwepo kwa changamoto ya ajira Zanzibar kuna haja ya kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja kati ya Serikali na sekta Binafsi katika kutatua changamoto hiyo iliyopo.
Aidha, Dk. Shein alieleza namna Serikali inavyofanya juhudi ya kuongeza thamani ya mazao ya biashara sambamba na kuiimarisha sekta ya kilimo, uvuvi, viwanda na utalii.
Rais Dk. Shein alisisitiza haja ya kuyalinda mazao na bidhaa za Zanzibar na kueleza umuhimu kwa wananchi kujali na kuthamini bidhaa na mazao yao ya nyumbani.
Nae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd alieleza haja kwa wamiliki wa hoteli, kuwalipa kwa wakati muwafaka vijana wanaojiajiri ambao huuuza bidhaa zao zikiwemo za kilimo kwa ajili ya matumizi katika hoteli hizo.
Nae Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Salum Ali alieleza umuhimu wa mashirikiano ya pamoja kati ya sekta Binafsi na Serikali pamoja na kuitaka sekta Binafsi kuwainua wafanyabiashara wadogo wadogo.
Nae Katibu Mtendaji wa Baraza la Biashara la Zanzibar Bakari Ally Bakari alieleza kuwa kauli mbiu ya Jukwaa la Biashara la 9 la Zanzibar mwaka huu ambalo linatarajiwa kufanyika Novemba 24, 2018 kuwa ni “Mashirikiano baina ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi katika kukuza ajira kwa vijana”.
Nae Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Khamis Mussa alieleza miradi mbali mbali ya maendeleo ambayo Serikali imetekeleza na mengine inaendelea kutekeleza na kueleza haja kwa Sekta Binafsi kuifahamu ukiwemo uwamuzi wa Serikali kununua meli ya mafuta ili kupunguza changamoto inayojitokeza mara kwa mara na upanuzi wa uwanja wa ndege wa Pemba na mengineyo.
Mkutano huo ulitolewa muhtasari wa Makala zitakazowasilishwa katika Jukwaa hilo ikiwemo Vijana na fursa za kiuchumi, fursa za ajira katika sekta ya kilimo, fursa za ajira katika uvuvi, fursa za ajira katika sekta ya utalii na kiutamaduni, fursa za ajira katika sekta ya utalii na fursa za ajira katika sekta ya viwanda.
Wajumbe wa Mkutano huo wakichangia juu ya makala hizo walieleza kuwa fursa nyingi za vijana katika sekta za maendeleo na umuhimu wa kuwasaidiwa kwani wengi hujishughulisha na shughuli za uzalishaji kwa kuigana hasa katika sekta ya kilimo.
Wajumbe hao walieleza kuwa kwa wale watu wenye uwezo wa kuekeza ni vyema wakawasaidia vijana kwa kuwapa taaluma juu ya soko la bidhaa zao huku wakieleza umuhimu wa vijana wajasiriamali kushiriki maonyesho ya ndani na nje ya nchi.
Walieleza kuwa suala la vijana ni muhimu na linatakiwa kuzungumzwa kwa umakini na undani zaidi hasa kuwepo kwa mashirikiano ya pamoja kati ya sekta binafsi na sekta ya umma katika kuwasaidia vijana katika soko la ajira.
Kwa upande wa sekta binafsi wajumbe hao walieleza kuvutiwa kwao na hatua za Serikali za kuwa na malengo na azma ya kushirikiana na sekta Binafsi katika kuwasaidia vijana katika soko la ajira huku wakieleza hatua zinazochukuliwa katika kuiimarisha Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenyeviwanda na Wakulima Zanzibar.
Walieleza kuwa vijana wengi wa Zanzibar hivi sasa wameamka na wameamua kubadilika hivyo kuna haja kwa sekta binafsi kutoa ushirikiano kwa vijana wajasiriamali hasa wale wanaojishughulisha na sekta ya kilimo, utalii, uvuvi, viwanda na nyenginezo sambamba na kuwapa taaluma itakayowasaidia.
Hata hivyo, mkutano huo ulieleza mikakati iliyowekwa ya kuimarisha sekta ya utalii, utalii na utamaduni, kilimo, uvuvi na viwanda na namna vijana watakavyoshirikishwa kwa lengo la kupata ajira sambamba na kuishirikisha sekta binafsi.
Mkutano huo ambao pia, uliwashirikisha wajumbe waalikwa wakiwemo Mawaziri na Makatibu Wakuu na viongozi wengine wa (SMZ) ni maandalizi ya mkutano wa maandalizi ya Jukwaa la Tisa la Biashara la Zanzibar linalotarajiwa kufanyika Novemba 24, 2018 katika ukumbi wa Idrissa Abdulwakil Kikwajuni mjini Zanzibar.
Katika mkutano huo pia, kuliwasilishwa hoja kutoka sekta Binafsi katika kukuza ushirikiano baina ya Serikali na sekta Binafsi, hoja kutoka Serikalini katika kukuza ushirikiano baina ya Serikali na sekta Binafsi, taarifa ya uundwaji wa Mabaraza ya Mikoa pamoja na mapendekezo ya ratiba ya Jukwaa la Tisa la Biashara la Zanzibar.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar