Mkurugenzi wa ufundi wa shirikisho la soka nchini (TFF), Ammy Ninje amesema katika kuhakikisha soka la Tanzania linapiga hatua chini ya uongozi wake, ataanza na vipaumbele vitatu ambavyo ndio hitaji kubwa la taifa.
Ninje ameweka bayana kuwa ataanza kwa kutengeneza falsafa ya mpira, kuongeza makocha wenye sifa kufundisha ligi kuu na kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni.
Mipango hiyo ya Ninje ni ishara ya kuanza kazi yake rasmi ambapo ameeleza kuwa, endapo mambo hayo yatafanywa kwa ufanisi yatapelekea timu za taifa na vilabu kufanya vizuri kwasababu kutakuwa na mfumo mmoja wa kucheza.
“Nataka kutengeneza ‘philosophy’ ya mpira wa Tanzania, maana tunatakiwa kujua tunataka kucheza mpira wa aina gani kwa sababu wamepita walimu wengi tangu miaka ya 1980 lakini hadi leo hatuna ‘philosophy’ na huenda ndio sababu ya kutofanya vizuri”, amesema.
Ninje pia amesema katika timu 20 za ligi kuu ni walimu 7 tu ndio makocha wakuu wakati wengine wasaidizi jambo ambalo nalo linalinyima taifa kuwa na utamaduni wake kuanzia ngazi ya vilabu kwani makocha wa kigeni huja na mifumo yao.
Kwa upande wa wachezaji wa kigeni Ninje amesema anatamani kuona vilabu vikitumia wachezaji wa ndani zaidi hivyo anafikiria kubadili sheria ya wachezaji wa nje kutoka 10 ilivyosasa hadi watano tu.
Aidha amesema kwa upande wa timu za taifa za vijana kama U17, U20 na U23 tayari zimeshaanza kuonesha mfano lakini tatizo linabaki kwenye vilabu ambavyo wachezaji hao wanacheza mara nyingi wamekuwa hawapewi nafasi.