HABARI KUU
Na Benny Mwaipaja, Kondoa
ZAIDI ya wakazi
elfu 16 wa vijiji vitatu vya Mauno, Makiranya na Kinyasi-Majengo,
katika Jimbo la Kondoa Vijijini mkoani Dodoma wameondokana na adha ya
kukosa maji baada ya kuzinduliwa kwa visima viatu vya maji vilivyojengwa
kwa msaada wa wahisani kutoka nchini Uturuki kupitia ubalozi wa nchi
hiyo hapa nchini
Akizungumza
wakati wa hafla ya uzinduzi wa visima hivyo katika Kijiji cha Mauno,
Kata ya Bumbuta, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mbunge
wa Jimbo la Kondoa Vijijini Dokta Ashatu Kijaji, amesema kuwa
kuzinduliwa kwa visima hivyo kunalifanya jimbo lake lifikishe visima 41
hatua ambayo amesema itapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la maji katika
jimbo lake.
Dkt. Kijaji
ameushukuru Ubalozi wa Uturuki kwa kuratibu msaada huo wa zaidi ya Dola
za Kimarekani elfu 36, sawa na shilingi milioni 81, zilizotumika
kuchimba visima hivyo pamoja na kuweka miundombinu mingine zikiwemo
jenereta zinazotumika kusukuma maji hayo na kuwezesha upatikanaji wa
maji hayo.
"Hivi sasa
ujenzi wa visima 15 kati ya 25 vinavyojengwa na Serikali kupitia Wizara
ya Maji unaendelea huku wahisani wakiwa wametujengea visima 36 hivyo
kufikisha idadi ya visima 61 katika kipindi cha miaka miwili tu tangu
Serikali ya Awamu ya Tano ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli aingie
madarakani hali ambayo haijawahi kutokea na lengo letu ni kuhakikisha
kuwa vijiji vyote 84 vinapatiwa huduma ya maji ifikapo mwaka 2020"
Alisisitiza Dkt. Kijaji
Diwani wa Kata
ya Bunbuta Bw. Bashiru Mtolo na mkazi mmoja wa kijiji hicho Bi. Khadija
Hussein wamesema kuwa tatizo la maji katika kijiji cha Mauno lilikuwa
kubwa na kuwalazimisha wanawake na watoto kwenda umbali mrefu kusaka
maji kwa ajili ya matumizi yao ya majumbani pamoja na kunywesha mifugo.
"Tunaushukuru
Ubalozi wa Uturuki kwa msaada wao huu mkubwa na Mbunge wetu kwa
ufuatiliaji wake wa karibu uliowezesha kupatikana kwa visima hivi na
vingine ambavyo vimesaidia kwa kiwango kikubwa kutatua kero ya maji na
tunaamini mpaka kufikia mwaka 2020, matatizo ya maji katika wilaya yetu
ya Kondoa litakuwa historia" alisema Diwani Mtolo.
Naye
Mwakilishi na Mwambata wa Ubalozi wa Uturuki hapa nchini Sheikh
Muhammad Cicek ameeleza kuwa msaada wa Dola elfu 36 zilizotumika kujenga
miradi hiyo mitatu ya visima vya maji umetolewa na wahisani mbalimbali
wa Uturuki ikiwa ni kuenzi uhusiano wa muda mrefu kati ya Uturuki na
Tanzania.
Alisema
kukamilika kwa miradi hiyo ya maji kutasadia kuwawezesha akina mama na
wananchi wa Kondoa kwa ujumla kufanya shughuli nyingine za maendeleo
badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji ambayo hata hivyo hayakuwa
safi wala salama.