George Bush Senior, kama alivyofahamika sana, alifariki dunia mwendo wa saa nne na dakika kumi usiku (saa kumi na dakika kumi GMT), msemaji wa familia hiyo ametangaza.
Alikuwa rais kati ya mwaka 1989 na 1993 baada ya kuongoza kwa mihula miwili kama makamu wa rais chini ya Rais Ronald Reagan.
Aprili, alilazwa hospitalini akiwa na maambukizi kwenye damu lakini akatibiwa na kuruhusiwa kuondoka hospitalini.
George Herbert Walker Bush amefariki miezi saba tu baada ya kifo cha mke wake Barbara.
Viongozi wamekuwa wakituma salamu za rambirambi na kumkumbuka mwanasiasa huyo, wakiongozwa na Rais wa sasa wa Marekani Donald Trump aliyemsifu kwa “uhalisiwa wake, ucheshi na kujitolea kwake kudumisha imani, kwa familia na kwa taifa.
Bendera katika ikulu ya White House zitapepea nusu mlingoti huku mipango ya mazishi ikiendelea.
Kuapishwa kwa George H W Bush kuwa Rais wa Marekani mnamo Januari 1989 kulikuwa kilele cha ufanisi wake katika siasa.
Alikuwa ameandaliwa kwa muda mrefu kupitia mafunzo ya kiwango cha juu, na kupandishwa madaraka mara kwa mara kabla ya kuishia Ikulu ya White House.
Rais huyu wa 41 wa Marekani alifanya kazi kama makamu wa Rais wa Ronald Reagan kwa miaka minane.
Alikuwa Makamu wa Rais wa kwanza aliyekuwa afisini kufanikiwa kuchaguliwa kuwa Rais katika kipindi cha zaidi ya miaka 150.
Utawala wake unahusishwa sana na siasa za wakati ule ambapo Ukomunisti ulikuwa ukiporomoka Ulaya Mashariki na kusambaratika kwa Muungano wa Usovieti (USSR) ambapo Marekani iliachwa ikiwa taifa kubwa zaidi kiuchumi na kiviwanda duniani.
Uongozi wake ulisaidia kurejesha hadhi ya Marekani kwa dunia nzima na kurejesha heshima yake kufuatia uvamizi wa Marekani nchini Vietnam, ulioiletea Marekani aibu.
Hata hivyo alilaumiwa kwa kupuuza maswala ya ndani ya Marekani na kwa kupuuzilia mbali ahadi aliyoitoa wakati wa kampeni ambapo aliahidi kuwa hataongeza kodi.
Kupuuzilia mbali kwa ahadi hiyo kulimfanya ashindwe katika uchaguzi uliofuata na Bill Clinton wa chama cha Democratic mwaka 1992.
Maisha ya kisiasa
- 1966: Alishinda kiti katika Bunge la Wawakilishi
- 1971: Nixon amteua kuwa balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa
- 1974: Ateuliwa kuwa Balozi wa Marekani katika ubalozi mpya nchini Uchina
- 1976: Ford amteua kuwa mkurugenzi wa shirika la upelelezi la CIA
- 1981-1989: Makamu wa Rais wa Ronald Reagan
- 1989-1993: Rais wa Marekani; aongoza Marekani katika Vita vya Kwanza vya Ghuba; akabiliana na hali ya kuporomoka kwa Ukomunisti Ulaya Mashariki.
George Herbert Walker Bush alizaliwa Julai 12, 1924 katika Milton, Massachusetts. Baba yake alikuwa mwekezaji katika benki na baadaye akawa Seneta wa Marekani.
Alijitolea kupigana katika jeshi la wanamaji Vita Vikuu vya Pili vya Dunia baada ya kushambuliwa kwa Pearl Harbor. Alipata mafunzo ya kuendesha ndege za kivita kabla ya kupewa majukumu katika vita katika Bahari ya Pacific ambapo alishiriki katika vita dhidi ya Wajapani katika Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Akiwa na umri wa miaka 18 pekee, ambapo inawezekana alikuwa miongoni mwa marubani wachanga sana Wamarekani, alipewa kazi ya urubani wa ndege za kijeshi za kuangusha mabomu zinazoruka angani kutoka kwa meli kubwa za kivita.
Ndege yake ilitunguliwa Septemba 1944 alipokuwa akielekea kuangusha mabomu. Ndege yake ilijaa moshi na ndimi za moto zilianza kuteketeza mbawa zote mbili. Anakumbuka akisema: “Mungu wangu! Ndege hii italipuka.”
Aliendelea kuendesha ndege hiyo na kuangushia mabomu shabaha zake kadhaa. Aliwaamuru wanahewa wawili aliokuwa nao wajisalimishe kwa kuruka kwa miavuli kutoka kwenye ndege hiyo lakini wote wawili hawakunusurika.
Bush alisongwa na moshi lakini akavalia mwavuli pia na kuruka kama wenzake. Alianguka kwenye kisiwa kimoja baada ya kugongwa kichwa chake na sehemu ya nyuma ya ndege kwa sababu ya upepo akiruka.
Alifanikiwa kufikia boya na akaanza kulielekeza kama ngalawa akitumia mikono yake kama makasia kutoroka visiwa vilivyokuwa mikononi mwa Wajapani.
Alikuwa na bahati ajabu, kwani kabla hajakwenda mbali nyambizi iliibuka alikokuwa na kumwokoa. Nyambizi hiyo iliendesha shughuli zake kwa utaratibu sana na walirekodi kila kitu kwa filamu.
Baada ya kuondoka kwenye kikosi cha wanamaji mwaka 1945 kwa heshima, Bush alimwoa msichana mwenye umri wa miaka 18, Barbara Pearce.
Ndoa yao ilidumu miaka 72 na wakafanikiwa kuwapata watoto sita.
Mwana wao wa kwanza, ambaye baadaye alikuwa Rais George Walker Bush, alizaliwa mwaka mmoja baadaye.
Awali Bush alikuwa amepewa nafasi kuendelea na elimu katika Chuo Kikuu cha Yale kabla ya kusajiliwa katika kikosi cha wanamaji. Mara tu alipotoka jeshini mwaka 1945 baada ya vita kumalizika, alirudi katika chuo Kikuu na kukamilisha shahada yake katika sanaa.
Busha na familia yake kisha walihamia Texas ambako alitumia uhusiano mzuri wa kibiashara wa baba yake kupata kazi katika sekta ya mafuta.
Kabla ya kufikisha miaka 40, tayari alikuwa milionea.
Bush na mkewe Barbara walisononeka sana baada ya binti yao wa pekee kugunduliwa kuwa na maradhi ya kansa ya kukosekana kwa damu mwilini, kwa Kiingereza Laukaemia.
Robin alipelekwa hospitalini kutokana na uchovu mwilini lakini Bush na mkewe walishtushwa na maelezo ya daktari.
Familia hiyo ilishtushwa na kifo cha Robin miezi michache baadaye.
Pigo la tukio hilo lilijitokeza baada ya kifo cha Barbara Bush alipofariki miaka 65 baadaye, familia hiyo iliweka bango lenye maandishi yaliyosema “Tafadhali mama, mkumbatie Robin kwa niaba yetu.”
Uhafidhina
Mawazo ya kikazi ya George Bush yalibadilika na kuingilia siasa.
Baada ya kuhudumu kwa muda kama mwenyekiti wa tawi la chama cha Republican eneo la Texas, alifanya uamuzi mgumu. Alishindana kutaka kuteuliwa kama mgombea wa Useneta wa chama chake cha Republican katika jimbo la Texas.
Seneta wa eneo hilo wa chama cha Democratic aliwaambia watu kuwa Bush alikuwa mwanasiasa wa msimamo mkali wa mrengo wa kulia.
Mwanachama huyo wa Democtatic alipata asilimia 56 ya kura zilizopigwa zikilinganisha na asilimia 43 za Bush. Bila kukata tamaa Bush aligombea kiti cha bunge la wawakilishi na akashinda kiti mwaka 1966. Alihudumu mihula mbili.
Rais Richard Nixon alimshawishi Bush kugombea Useneta tena mwaka 1970 lakini tena akashindwa na mgombea yule yule wa Democratic.
Rais Nixon alimteua Bush kuwa balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa 1971 na kisha akawa mwenyekiti wa chama cha Republican.
Wakati Nixon alipolazimishwa kujizulu 1974, Bush alifanya kila juhudi kumponya baadhi ya makovu yaliyosababishwa na kashfa ya Watergate, ambapo alitumia muda wake mwingi kuwatetea wagombezi wa Republican kwa kufanya ziara maeneo mbalimbali nchini humo.
Mwisho wa mwaka alienda Uchina kuwa balozi katika ubalozi mpya wa Marekani nchini humo.
Baada ya kuwa nchini Uchina kwa mwaka mmoja pekee, Rais Gerald Ford alimrejesha nyumbani Bush na kumteua kuwa mkurugenzi wa shirika la upelelezi la CIA, shirika ambalo lilikuwa limekabiliwa na msururu wa kashfa kuhusiana na operesheni za usiri mkubwa nje ya nchi pamoja na kuwapeleleza raia wa Marekani bila idhini.
Kutumwa kwake CIA kulitokea wakati ambapo mkewe Barbara alikuwa amezidiwa na ugonjwa wa kiakili.
Mke wake aliandika kwenye kitabu kuhusu maisha yake kwamba angelielekeza gari lake pembeni mwa barabara akiogopa kugonga mti au magari yaliyokuwa yakienda upande ule mwingine. Hisia hizo baadaye zilitokomea.
Bush aliondoka CIA baada ya Ford kuondoka madarakani na mwaka 1978 akaanza kufanya kampeni ya kutaka kuteuliwa kuwa mgombea wa urais wa chama chake katika uchaguzi wa mwaka 1980.
Alizuru kote nchini akieleza juu ya msimamo wake wa uhafidhina wa kadri. Kufikia 1980 ilionekana wazi kuwa ni yeye pekee aliyebakia ambaye angetoa ushindani mkali dhidi ya Ronald Reagan.
Mara tu alipojiingiza katika kinyang’anyiro cha kisiasa, Bush aligundua kuwa kulelewa kwake katika maisha ya hadhi awali kungekuwa kama gharama kwake kisiasa.
“Kuna kosa gani katika kufaulu maishani, ” Bush aliuliza wakati ule. Aliongezea :” Kuna kosa gani kuwa na elimu nzuri? Kuna kosa gani ikiwa nilifaulu maishani na katika biashara zangu au kuwa balozi mzuri nchini Uchina au katika Umoja wa Mataifa au kufanya kazi nzuri katika CIA. Haya yote nimefanya mimi. Najua wengine watasema ni kujigamba lakini hiyo ndiyo rekodi yangu.”
Aliposhindwa na Reagan alikuwa na bahati nyingine ya kumliwaza. Aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa reagan ambapo alihudumu kama makamu wa Rais kwa miaka minane, ambapo ilikuwa ni kama kipindi cha mafunzo ya kujiandaa kuwa Rais.
Katika uchaguzi wa 1988 ambapo alishinda na kuwa Rais, George H W Bush alifanya makosa mawili makubwa.
Kosa la kwanza ni kumchagua Makamu wa Rais asiyejulikana: Dan Quayle, aliyekuwa Seneta wa hadhi ya chini kutoka Indiana. Quayle alijulikana kimataifa zaidi kutokana na makosa aliyoyafanya kwenye hotuba na mazungumzo yake.
Kosa la pili lilikuwa kuahidi wakati wa kampeni kuwa hataongeza kodi wakati wa Kongamano kuu la chama cha Republican la kuidhinisha mgombea urais mwaka 1988..
Alipokuwa anamshambulia mpinzani wake wa chama cha Democratic Michael Dukakis kuhusu sera yake ya kifedha, alitoa ahadi hiyo ambayo baadaye ilichangia kumuondoa madarakani.
‘ aliwaambia wajumbe waliokusanyika. ‘Hakuna kodi mpya.’
Baada ya kampeni kali sana kuwahi kufanyika nchini humo, Bush alikuwa Makamu wa Rais wa kwanza kuchaguliwa kuwa Rais tangu kuchaguliwa kwa Martin Van Buren kuwa rais mwaka 1836.
Wakati huu ulikuwa wa kipekee kwa sababu hapo ndipo Serikali ya Muungano ya Usovieti uliporomoka na ‘Ukuta wa Chuma’ uliodaiwa kutenganisha Ulaya Mashariki na Ulaya Magharibi ‘ukabomoka’.
“Upepo mpya unavuma, na dunia iliyotiwa upya matumaini na uhuru inaonekana kuzaliwa; kwani ndani ya moyo wa binadamu, kama si kwa kweli kabisa katika uhalisia, enzi ya dikteta imefikia kikomo,” alitangaza akiwa kwenye vidato vya jengo la Capitol, makao makuu ya bunge la Congress.
Mtihani mkubwa kwa Bush ulilijitokeza wakati Iraq iliposhambulia Kuwait kwa ghfula Agosti 1990.
Bush aliunda muungano wa kijeshi wa kimataifa kushambulia Iraq nchini Kuwait kuhakikisha majeshi ya Saddam Hussein yanatimuliwa huko.
Wakati huo huo alianzisha kikosi maalumu cha wanajeshi wa Marekani kupiga kambi nchini Saudi Arabia, eneo zuri kuweka wanajeshi wa kukabiliana na maadui wa Marekani katika Ghuba.
Busha alichelewesha kushambulia Iraq nchini Kuwait kwa sababu alikuwa akisubiri kupata idhini ya Umoja wa Mataifa. Lakini alishutumiwa vikali na aliyekuwa Waziri Mkuu Uingereza Margaret Thatcher.
“Ni sawa George lakini huu si wakati wa kuyumbayumba,” ndivyo alivosema Bi Thatcher katika simu aliyompigia Bush usiku wa manane kutoka Downing Street.
Vita vilivyofuata viligeuka kuwa ushindi mkubwa kwa Marekani na wataalamu wa kijeshi wa Marekani walipongezwa na taifa kwa jumla lilifurahia hadhi iliyotokea kwa jeshi baada ya mapigano hayo.
Chini ya uongozi wa Marekani mapigano hayo yaliendelea kwa saa 100 pekee.
Ushindi huo uliimarisha hadhi aliyokuwa nayo Rais Bush licha ya kwamba kikosi hicho cha muungano hakikuingia Baghdad kwenyewe ambapo kilimwacha Saddam Hussein kuendelea kuwa mamlakani.
Kumpindua Saddam Hussein na serikali yake kulitekelezwa na mwanawe Bush baadaye.
Ingawa umaarufu wake ulipanda na kufikia asilimia 90 wakati mmoja, uamuzi wa Bush wa kutilia mkazo masuala ya nje ya nchi kulifanya wakosoaji wake wengi kusema kuwa alikuwa akipuuza masuala ya nyumbani na kusababisha maisha kuwa magumu sana kiuchumi tangu vita Vikuu vya Pili vya Dunia.
Alishinikizwa sana na wanachama wa Democratic ambao walidhibiti bunge, lakini Bush alisisitiza kwamba makali ya mgogoro wa kiuchumi wa wakati huo yalikuwa yamepita.
“Tutaliondoa taifa hili kutoka katika ugumu wa kiuchumi,” Bush aliahidi. “Hatua kwa hatua na wale wanaotaka kutuchelewesha au kutuzua bora watuondokee njiani.”
Lakini taifa halikumsadiki na kisha akafanya jambo ambalo alikuwa ameahidi kuwa hatalifanya: aliongeza ushuru.
Uchaguzi wa 1992 ulikuwa na matokeo mabaya sana. Wasimamizi wa kampeni yake hawakuwa na mpango mzuri na wakati huo huo alikabiliwa na upinzani mkali katika uchaguzi wa mchujo kutoka kwa Pat Buchanan katika chama chake cha Republican.
Wakati wa uchaguzi Bush hakuwa na nguvu za kukabiliana na mpinzani wake kutoka chama cha Democratic, Bill Clinton, aliyekuwa mchanga na aliyependwa na watu.
Bush baadaye alikiri kuwa bidii aliyokuwa nayo Bill Clinton, gavana wa umri mdogo kutoka jimbo la Arkansas, na ambaye alitoa matumaini ya ndoto mpya kuu ya Marekani, yeye Bush hangeweza kukabiliana nayo.
Picha iliyoonyesha wazi yaliyokuwa yakitokea ilikuwa wakati wa ziara yake nchini Japan ambayo haikufanikiwa. Rais Bush alilakiwa na chakula maalumu cha wageni lakini akatapika kwanza mezani kabla ya kuzimia jambo ambalo wenyeji wake hawakuonekana kulifurahia. Bush baadaye alishindwa vibaya sana uchaguzini.
Miaka yake ya baadaye aliitumia akitalii dunia na kutekeleza wajibu wake na kiongozi wa zamani wa nchi.
Ingawa alijivunia kwamba mwanawe George W Bush alifanikiwa kuingia White House, uhusiano kati ya wanaume hao wawili ulidaiwa kutokuwa mwema.
Bush aliadhimisha miaka 90 tangu kuzaliwa Juni mwaka wa 2014 kwa kuruka na mwavuli kutoka kwa ndege karibu na nyumba aliyoitumia kwa ajili ya msimu wa joto katika eneo la Kennebunkport, Maine.
Alianza kuonekana mara chache hadharani na akaanza kuishiwa na nguvu hivi kwamba akaanza kutumia kiti cha magurudumu baada ya kushikwa na maradhi yanayohusiana na uzee ya Parkinson. Hakuweza kutumia miguu yake baada ya hapo.
Wanawake kadhaa wamewahi kumlaumu kwa kuwafanyia vitendo visivyo vya heshima siku zilizopita.
Msemaji wake, Jim Mcgrath, alikiri kuwa siku zilizopita Bwana Bush amewahi kuwagonga wanawake kwa mkono kwenye makalio katika kitendo alichokusudia kuwa mzaha.
Rais huyo wa zamani alikanusha kuwa aliwahi kumpapasa mwanamke yeyote lakini akasema kuwa anamwomba msamaha yeyote ambaye huenda alimwudhi kwa kitendo sawa na hicho.
Alifiwa pia na kipenzi chake cha roho – Barbara baada ya ndoa yao kudumu zaidi na miaka 70. Ibada ya wafu ya Barbara ilihudhuriwa na Marais wastaafu, Bill Clinton na Barack Obama – ingawa Rais Trump hakujitokeza.
Alipokuwa Rais alifanya kazi kikamilifu kama Menaja na wala sio mtu aliyekuwa akijifunza kuwa kiongozi.
Alidharauliwa mara nyingi na wananchi waliomdhania kuwa mtu mwenye maringo asiyeelewa maisha ya raia wa kawaida.
Uongozi wake katika maswala ya kigeni ulifaulu sana hasa katika kukabiliana na mashambulizi ya Iraq nchini Kuwait na kukabiliana na kuporomoka kwa utawala wa Kikomunisti.
Uongozi wake wa maswala ndani ya nchi haukupongezwa sana kwa sababu wakosoaji wengi kusema kwamba ni kiongozi aliyechanganyikiwa katika masuala ya kiuchumi.
Lakini kama mtu Binafsi, George Herbert Walker Bush, atakumbukwa kama mtu mstaarabu, mpenda familia, ambaye kusema kweli hakupendelea sana makabiliano na matusi katika masuala ya kisiasa.
Alinukuliwa akisema kuwa: “Kwa kuwa tunashindania kiti haimaanishi kuwa sisi ni maadui.”
Aliongeza kwamba: “Siasa hazipaswi kuwa mbovu na bila heshima, ili eti ziwe ni siasa.”