Na. Immaculate Makilika – MAELEZO
Serikali imesema mfumo mpya wa visa na vibali vya ukaazi vya kielektroniki unatajwa kuwa na faida lukuki kwa nchi ikiwemo kukuza sera ya diplomasia ya uchumi, sera ya viwanda, kusaidia ongezeko la watalii wanaokuja nchini pamoja na kuongeza ukusanyaji wa madurufu ya Serikali.
Akizungumza jana, jijini Dar es salaam, wakati akizindua mfumo wa visa na vibali vya ukaazi vya kielektroniki, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa, alisema kuwa mfumo huu mpya unatarajia kufikia malengo ya Serikali ya kukuza diplomasia ya uchumi, kuchochea kasi ya maendeleo na uchumi wa viwanda, sambamba na hilo raia wa kigeni wanaweza kuomba huduma hiyo wakati wowote na mahali popote duniani.
“Ni imani yangu kuwa mfumo huu mpya utatatua changamoto zote zilizokuwepo awali, lakini pia utarahisisha upatikanaji wa huduma kwa raia wa kigeni. Ni muhimu kwa mfumo huu kuunganishwa na mifumo mingine ya Idara ya Kazi, Kituo cha Uwekezaji, Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), pamoja na Mfumo wa Malipo wa Kieletroniki Serikalini (GePG), ambayo itamsaidia mteja kupata huduma kwa urahisi bila usumbufu wowote” alisema Waziri Mkuu
Waziri Mkuu Majaliwa, aliongeza kuwa mfumo huo utasaidia kutoa huduma kama ambavyo Serikali imekusudia, sambamba na kusaidia nchi katika masuala ya ulinzi na usalama.
Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Augustine Mahiga alisema kuwa mfumo huo utasaidia kukuza sekta ya utalii, ambapo kwa mwaka watalii milioni moja hadi mbili pekee wanafika nchini, ambapo fedha za kigeni zinapatikana katika sekta hiyo ya utalii.
“Matarajio yangu kwamba mfumo huu mpya wa visa na vibali vya ukaazi vya kielektroniki, utasaidia kuboresha na kuvutia wawekezaji, sambamba na kuleta watalii nchini”
Pia, Waziri Mahiga alisema Wizara yake itaelimisha Jumuiya ya Mabalozi kuhusu huduma hiyo, ikiwa ni sambamba na kufanya diplomasia ya uchumi.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu wa Uhamiaji nchini, Dkt. Anna Makakala alisema kuwa mfumo huo mpya wa visa na vibali vya ukaazi vya kielektroniki utasaidia kuimarisha usalama, uwekaji wa kumbukumbu, pamoja na kuwezesha Idara ya uhamiaji kupata taarifa na kuzifanyiakazi kabla ya mgeni kuwasili nchini, pamoja na kukusanya madurufu ya serikali bila upotevu
“Kuanzia Januari 31, mwaka 2018 hadi Novemba 25, 2018 jumla ya hati mpya za kusafiria za kielektroniki 55, 177 zimetolewa, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 7 zimepatikana kutokana na malipo ya hati mpya za kusafiria za kielektroniki” alisema Kamishna Mkuu wa Uhamiaji
Aidha, ifikapo Januari 2019 huduma ya upatikanaji wa hati mpya za kusafiria za kielektroniki itapatikana katika balozi zote za Tanzania ili kuwarahisishia huduma watanzania au raia wa kigeni walioko nje ya nchi.
Mradi wa Uhamiaji Mtandao unaohusisha mfumo wa hati ya kusafiria ya kielektroniki, mfumo wa visa na vibali vya ukaazi vya kielektroniki ambayo ni awamu ya pili, pamioja na mfumo wa kuzuia na kudhibiti wahamiaji haramu wanaoingia nchini.