Ni jambo la mazoea sasa mji wa Unguja kuwa na uhaba wa mafuta ya Petroli au Dizeli katika vipindi fulani Fulani.
Wachambuzi wa mambo wanashangazwa na hali hiyo, wakiziangalia takwimu za ukubwa wa eneo, matumizi ya mafuta, harakati za wananchi, wanajiuliza inakuaje uhaba wa mafuta unatokezea?
Labda tujiulize masuala kadhaa, Je tunatatizo la uwezo wetu wa bandari kushindwa kuhimili ukubwa wa meli za mafuta, Je matangi yetu ni dhoof-ul-haali na uwezo wake wa kilita si chochote si lolote kwa uwiano wa matumizi yetu, Je makampuni yanayoleta hayana fedha za kufanya biashara hiyo na inawezekanaje makampuni yasiwe na fedha. Watu wenye akili za kawaida tu wanajua utajiri wa mafuta ulivyo. Nenda vibarazani na maskani watakavyokusifia utajiri uliopo bara Arabu. Watakueleza waziwazi chanzo cha utajiri huo ni mafuta.
Wananchi wamezoea hali na wanajua kila baada ya muda watakwenda kugombania mafuta ya bei ya ulanguzi na kukasimiwa lita. Je waendeshaji nao wamezoea hali? Wanang’ang’ania ‘status quo’. Na kama hawang’ang’anii kwanini mambo kangaja kila wakati yaja.
Mwanataaluma Peter Senge katika kitabu chake cha ‘Five Discipline’ amezungumzia sana juu ya Taasisi inayosoma mambo na kuyatambua, mfano katika dhana moja ya hekaya ya Chura kwenye maji ya moto ‘Parable of the boiled frog’ anaeleza namna Taasisi inayoshindwa kuchukua hatua tokea awali ya jambo linapokuwa change na hutegemea italitatua litakapokuwa kubwa na linajulikana na kila mtu. Wapi! Yaguju! Ndiyo haya ya mafuta na hekaya ya Chura kwa dhana kwamba atabadilisha joto lake kwenye maji ya moto.
Wachunguzi wa ndani wa mambo katika sekta nzima ya uendeshaji wa biashara ya mafuta Zanzibar (si ya utafiti na uchimbaji) wanaeleza kwamba mara kwa mara karibu kila baada ya miezi miwili Zanzibar hukaribia au hukumbwa na tatizo la upatikanaji wa mafuta kutokana na pengine meli kuharibika, kukosa ukuta Dar es Salaam, kuchelewa kuagiza mafuta. Why? Kwanini?
Labda tutarajie ujenzi wa meli mpya ya mafuta ikimalizika! Labda tutarajie ujenzi wa bandari mpya ya mafuta mangapwani kumalizika! Labda lile jengo pale Maisara limalizike! Labda nini tena chengine, mkikumbuka mnitag!
Eti kampuni zinaagiza mafuta ya siku saba! Eti kampuni zina meli za kizamani! Eti tunajua uwezo wa hizi kampuni kifedha! Eti mikataba yao ya biashara ikoje!
Natambua juhudi za kubadilisha mfumo wa uagizaji wa mafuta zimefanyika lakini hazijaleta mafanikio. Sio BPS wala kampuni moja moja. Je ni dhana aliyoizungumzia Peter Senge ‘Problem of our own Thinking or System Thinking’.
Tutafute suluhisho wabobezi wa Uongozi wanaeleza kwamba ‘Challenging Status quo’. Tufyekelee mbali haya, Tusiyaache tu, kwani hakuna wengine, kwani hakuna namna nyengine. Tufanye vyengine. Chambilecho Rais wetu Daktari ALI MOHAMMED SHEIN tuache ‘Business as Usual’.