Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Zanzibar, leo tarehe 27 Mei, 2018 imefanya kikao chini ya Mwenyekiti wake ambae pia Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein.
Dk. Shein amewataka wajumbe wa Kamati Maalum ya NEC ya CCM Taifa Zanzibar kuendeleza kasi ya kuimarisha Chama kwa kutekeleza majukumu yao na kushuka kwa Viongozi na Wanachama wa ngazi mbali mbali ili CCM ishinde kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Kauli hiyo ameitoa leo hii katika Kikao cha Kamati Maalum, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Afisi Kuu ya CCM, Kisiwandui Zanzibar.
Pia kikao hicho kimepokea na kujadili taarifa za Viongozi Wakuu wa kitaifa, Wakuu wa Idara wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar pamoja na mikakati ya Chama kuelekea 2020.
Vile vile kikao hicho kimejadili mambo ya utendaji ya Chama Cha Mapinduzi ambayo yamepelekwa katika vikao vya ngazi za juu kwa ajili ya kujadiliwa.
Pamoja na hayo wajumbe wa Kamati hiyo wamepongeza kasi ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 inayotekelezwa kwa ufanisi zaidi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kikao hicho ni cha kawaida kwa mujibu wa Katiba ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 1977 Toleo la 2017,Ibara ya 108(2).
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Imetolewa na,
CATHERINE PETER NAO
KATIBU WA KAMATI MAALUM YA NEC
ITIKADI NA UENEZI CCM-ZANZIBAR.