Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi
wameishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweka ulinzi katika
maeneo ya Vivutio vya watalii ili kuwawezesha watalii wanaotembelea
vivutio hivyo kuendelea kuwa katika hali ya usalama na amani.
Wakiuliza maswali ya Nyongeza katika kikao
cha Baraza la wawakilishi Chukwani nje kidogo ya Mji wa Zanzibar
,Wajumbe hao wamesema Zanzibar ina sehemu nyingi zenye vivutio vya
watalii lakini vivutio hivyo havina ulinzi wa kutosha.
Wamesema sehemu hizo zitakapo wekewa ulinzi
na kuimarishwa kwa hali ya Usalama watalii wataongezeka na kuongeza
upatikanaji wa mapato ya Nchi.
Kwa Upande wake Naibu waziri wa wizara ya
Habari,Utalii,Utamaduni na Michezo Chumu kombo Khamis amesema kutokana
na umuhimu mkubwa wa watalii hapa Zanzibar Serikali italifanyia kazi
Suala hilo ili kuimarisha vyanzo vya mapato ya Ndani.
Amesema Mwaka Uliopita Sekta ya Utalii
ilifanikiwa kukusanya Shillingi million mia ambapo ni sawa na Shilingi
Millioni 10 kwa kila mwezi kutokana na Vyanzo vya mapato ya ndani
ikiwemo mapato yatokanayo na Matamasha mbalimbali ya Wanamuziki na
Watalii.
Naibu Chumu ametowa wito kwa wananchi
kuthamini na kuvitunza vivutio vya kitaliii vilivyopo Nchini pamoja na
kujenga utamaduni wa kuvitembelea ili kuongeza hamasa kwa wageni
wanaotoka nje ya Nchi pamoja na kuchangia pato la Taifa.