Hafla ya kugawa kamusi hizo imefanyika leo Februari 14, 2018 katika ukumbi wa mikutano wa Baraza la Kiswahili Zanzibar BAKIZA huko Mwanakwerekwe wilaya ya Mjini Unguja.
Akikabidhi kamusi hizo kwa vyombo vya habari Mwenyekiti wa baraza la kiswahili Zanzibar BAKIZA Dkt. Moh’d Seif Khatib amesema lengo la kugawa kamusi hizo ni kuwarahisishia waandishi kusambaza habari kwa kutumia lugha ya kiswahili fasaha na sahihi.
Dkt. Moh’d amesema kamusi itawasaidia waandishi kujua orodha ya maneno, maana za maneno, matamshi ya maneno n.k hivyo amewataka waandishi wasiridhike na kamusi ya lugha ya kiswahili kwa kiswahili walizopatiwa bali watafute na kamusi nyengine ili kuongeza weledi katika kazi zao.
Aidha Dkt. Moh’d ametumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa baadhi ya mashirika ya Serikali na binafsi yaliyochangia kufanikisha Kongamano la kiswahili kimataifa lililogharimu zaidi ya shiling milioni 28 za kitanzania ambapo asilimia 65 ya pesa hiyo ilichangwa kwa michango ya hiari.
Baadhi ya mashirika yaliyochangia ni Bodi ya mapato Zanzibar (ZRB), Mamlaka ya viwanja vya ndege Zanzibar, shirika la meli Zanzibar, shirika la bima Zanzibar, shirika la biashara la taifa Zanzibar, Kamisheni ya utalii Zanzibar, Shirika la simu la TTCL la muungano, kamisheni ya kiswahili ya Afrika Mashariki.
Nae mmoja miongoni mwa wandishi wa habari Muzne Ameir wa Zenj Fm Radio kwa niaba ya vyombo vya habari ameishukuru BAKIZA kwa kuona mchango wa waandishi wa habari katika kuieneza lugha ya kiswahili na kusema watatumia kamusi hizo kuelimisha jamii kwa kutumia lugha ya Kiswahili iliyo fasaha na kwausahihi.
Picha baadhi ya wawakilishi wa vyombo vya habari Zanzibar wakipokea kamusi la kiswahili fasaha kutoka kwa Mwenyekiti wa baraza la kiswahili Zanzibar BAKIZA Dkt. Moh’d Seif Khatib.