Meneja wa
Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) mkoa wa Dar es Salaam
Macdonald Maganga akitoa uamuzi wa wao kuwaweka kampuni ya udalali ya
Yono Auction kwa ajili ya kwenda kukamata wadaiwa sugu wote.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart, Scholastica Kevela
akitoa tamko la siku 14 kwa wadaiwa sugu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda
Vidogo (SIDO), kulipa madeni yao kabla ya chukuliwa hatua za kisheria
ikiwamo mali zao kupigwa mnada kufidia deni.
Meneja wa SIDO
mkoa wa Dar es Salaam Macdonald Maganga akiongoza wafanyakazi na
viongozi wa Yono kupita mlango kwa mlango wakati wakizundua kampeni ya
kudai madeni "LIPA DENI LAKO SIDO, KUWA MZALENDO'.
Wakiingia katika moja ya ofisi za mdaiwa wa SIDO.
Nae Mwenyekiti
wa Kuatamia mawazo ya wabunifu, Joseph Mlay ameiunga mkono SIDO kwa
hatua waliyochukua ya kuingia mlango kwa mlango katika kudai madeni yao.
Na Cathbert Kajuna - Kajunason/MMG.
Shirika la
Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO), mkoa wa Dar es Salaam imetangaza vita
kwa wale wadaiwa sugu kulipa madeni yao kabla ya chukuliwa hatua za
kisheria ikiwamo mali zao kupigwa mnada.
Kauli hiyo
ameitoa leo jijini Dar es Salaam, Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda
Vidogo (SIDO), mkoa wa Dar es Salaam Macdonald Maganga wakati akizindua
kampeni ya kukusanya madeni kwa wateja wao.
"Leo tunazindua
kampeni ya kukusanya madeni kwa wadaiwa sugu wote wa SIDO hatutakuwa na
huruma juu ya hili maana hawa ndiyo wanarudisha maendeleo ya shirika
nyuma, kuna waliokopa, walipanga kama haujalipa deni lako ujue tunakupa
siku 14 tu baada ya hapo sheria itachukua mkondo wake," amesema
Mkurugenzi Maganga.
Meneja
Macdonald Maganga amesema wadaiwa ni wale waliopewa maeneo maalumu ya
viwanda kwa ajili ya kufanyia kazi zao na waliopatiwa huduma ya fedha
kwa mkopo na kushindwa kurejesha kwa wakati.
“Kuna ambao
wamekaa miaka mingi au miezi mingi bila kurejesha fedha kwetu kama
shirika inatuathiri kwa sababu hatuwezi kuwahudumia wengine,” amesema
Maganga.
Maganga amesema wanadai jumla ya sh. milioni 350 kutoka kwa wadaiwa zaidi ya 77.
Kwa upande wa
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart,
Scholastica Kevela amewashukuru SIDO kwa kuweza kuwapa kazi hiyo ya
kuwakusanyia madeni na kuongeza kuwa hawata muonea huruma mdaiwa yeyote.
"Yono Auction
Mart tunatoa siku 14 kwa wadaiwa sugu wa Shirika la Kuhudumia Viwanda
Vidogo (SIDO), kulipa madeni yao kabla ya chukuliwa hatua za kisheria
ikiwamo mali zao kupigwa mnada kufidia deni,". amesema Mama Kevela.
“Kwa wadaiwa
wote wa SIDO, wanaoishi kwenye viwanda na nyumba za SIDO bila kulipa
pango, waliochukua mikopo na hawataki kurejesha kwa sababu wanazozijua
wao, mkono wa Yono uko kazini ni vyema wakachukua hatua wakalipa ili
kuondosha usumbufu,” amesema Kevela.
Mdaiwa Masoud
amedai hawafanyi makusudi kutolipa madeni ni kutokana na kodi kupanda
kila mwaka huku hali ya biashara ikiwa mbaya.
“Ukizingitia
soko la ushidani na hali ya bidhaa unashindwa kuuza kwa wakati kwa hiyo
tunalipa lakini hatulipi kwa wakati,” amesema.
Amedai
wamepangishwa kwa zaidi ya miaka 40 wakifanya shughuli zao na kama
wangekuwa hawalipi kwa kipindi chote wangefukuzwa hivyo ameiomba
serikali kutodhani kuwa wanapuuza kulipa madeni.