Waziri
wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (wa kwanza
kushoto) akitoa ufafanuzi wa idadi ya waandishi watakaohitajika katika
mkutano wakati wa mkutano wa majadiliano na Rais wa Shirikisho la Mipira
wa Miguu Duniani (FIFA) Bw.Gianni Infantino utakaofanyika mnamo
Februari 22, Mwaka huu na waandishi wa habari, katika mkutano wake na
Wahariri wa Habari za Michezo (hawapo pichani) nchini leo jijini Dar es
Salaam,Katikati ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na
Michezo Bibi Suzan Mlawi na Kulia ni Katibu Mkuu Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) Bw.Wilfred Kidau .
Katibu Mkuu Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania Bw.Wilfred Kidau
akitoa ufafanuzi kuhusu ajenda za mkutano wa Rais wa Shirikisho la
Mipira wa Miguu Duniani (FIFA) na CAF utakaofanyika nchini Februari
22,2018 katika mkutano na Wahariri wa Habari za Michezo nchini (hawapo
pichani) leo jijini Dar es Salaam.
Mwandishi wa Habari kutoka Gazeti la Nipashe Bi Somoe Ng’itu akiuliza
swali kuhusu utaratibu wa waandishi wa habari watakaofika Ikulu
kuripoti tukio la Rais wa Shirikisho la Mipira wa Miguu Duniani (FIFA)
kukutana na viongozi wakuu wanchi, kwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa
na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (hayupo pichani ) leo jijini Dar es
Salaam katika mkutano wa wahariri wa habari za michezo nchini.
Na Anitha Jonas – WHUSM
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Duniani (FIFA) kufanya mkutano
wa majadiliano na vyombo vya habari kumi na mbili vya ndani ya nchi.
Taarifa hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari
Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe katika mkutano na
wahariri wa habari za michezo uliyofanyika leo jijini Dar es Salaam.
‘’Huu ni utaratibu wa viongozi wa FIFA kufanya mkutano wa mazungumzo na
waandishi wa vyombo vya habari katika nchi wanazofanyia mikutano yao ya
kikazi kama ulivyo mkutano huu wanaotarajia kuufanya nchini Februari
22,mwaka huu,’’alisema Dkt. Mwakyembe.
Akiendelea kuzungumza katika mkutano huo Waziri Mwakyembe alieleza kuwa
Rais wa FIFA Bw. Gianni Infantino anatarajia kuwasili nchini alfajiri ya
saa nane usiku kuamkia Februari, 22 2018 ambayo ndiyo siku ya mkutano
na saa tatu asubuhi yake ataelekea ikulu kukutana na viongozi wakuu wa
nchi.
Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Bw.Wilfred Kidau
alitoa ufafanuzi kuhusu mkutano huu wa viongozi wa FIFA na CAF kuwa
umebeba ajenda mbalimbali ikiwemo kujadili kuhusu Maendeleo ya Soka la
Wanawake,Maendeleo ya Soka la Vijana,Utaratibu wa kusaidia Vilabu vya
soka pamoja na vipaumbele mbalimbali vya kukuza soka kwa nchi za Afrika.
‘’Mkutano huu wa FIFA unatarajia kufanyika katika ukumbi wa Mikutano wa
Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam (JNICC) na ni sawa na kikao cha
ndani ambacho kimelenga zaidi kujadili masuala ya maendeleo ya
shirikisho hilo kwa ajili ya kuandaa agenda za mkutano mkuu wa FIFA wa
dunia hivyo ombi kwa waandishi wa habari ni kuelewa dhana ya mkutano
siyo kuwa wamenyimwa fursa bali huo ndiyo utaratibu’,’alisema Bw. Kidau.
Pamoja na hayo Bw.Kidau alifafanua kuwa miongoni mwa vyombo
vitakavyopata fursa ya kushiriki majadiliano hayo baadhi yao watarusha
mazungumzo hayo mbashara katika vyombo vyao hivyo wadau wengine wataweza
kufuatilia tukio hilo moja kwa moja kupitia vyombo hivyo.
Halikadhalika Rais huyo wa FIFA anatarajia kuondoka nchini jioni mara
baada ya kumaliza mkutano mwake na kushiriki chakula cha jioni.